Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amezindua rasmi Awamu ya Pili ya Mradi wa Kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki leo katika Kampasi ya Mloganzila ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
Uzinduzi huu ni hatua muhimu katika juhudi za Tanzania kuboresha huduma za afya ya moyo na mishipa ya damu, pamoja na kuimarisha mafunzo ya kitaaluma na utafiti katika eneo hilo.
Awamu ya Pili ya mradi huu inahusisha ujenzi wa hospitali ya kisasa ya kufundishia ya moyo, mafunzo ya wataalamu bingwa na wabobezi wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, utayarishaji wa mitaala, na utoaji wa huduma bora na za kisasa za afya kwa jamii.
Katika hotuba yake, Prof. Mkenda alisisitiza dhamira ya Serikali ya kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ya elimu na afya ili kuboresha huduma kwa wananchi na kukuza utafiti wa kisayansi.
Alieleza kuwa kituo hiki kitakuwa kitovu cha ubobevu katika matibabu, mafunzo na utafiti wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, hivyo kusaidia kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa haya nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Appolinary Kamuhabwa, alisema kuwa mradi huu utasaidia kupunguza gharama za matibabu nje ya nchi, huku pia ukiwavutia wagonjwa kutoka mataifa mengine kutibiwa nchini, jambo ambalo litakuza dhana ya utalii wa tiba (medical tourism) na kuleta manufaa makubwa ya kiuchumi kwa taifa.
Mradi huu unatekelezwa na MUHAS na unagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 83.333 (ikiwa ni pamoja na mchango wa Serikali ya Tanzania).
Aidha, kabla ya uzinduzi huo, Prof. Mkenda alizindua pia kifurushi cha huduma za dharura kwa mama na mtoto kinachoitwa Breathing for Babies (BfB) pamoja na maabara ya mafunzo ya ujuzi kwa ajili ya kusaidia huduma hizo za dharura.