Kitengo cha utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET PIU) cha Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimefanya Kikao Kazi cha mapitio ya mwaka ya utekelezaji wa mradi (Annual Project Implementation Review Workshop) tarehe 20 – 24 Mei, 2024, Morogoro.
Katika ufunguzi wa Kikao Kazi hiki Mwenyekiti ambaye pia ni Msimamizi wa Ufuatiliaji na Utathmini wa Mradi, Dr. George Ruhago amesema madhumuni ni ya kikao ni kupokea taarifa za mradi, kufanya mapitio ya kazi za mradi na kupanga utekelezaji wa kazi za baadaye kulingana na Malengo ya Maendeleo ya Mradi.
Dr. Ruhago aliweza pia kuwapitisha washiriki wa kikao kazi hiki kwenye wasilisho kuhusu maendeleo ya mradi wa HEET MUHAS kwa ujumla tangu utekelezaji ulipoanza mwaka 2022 mpaka sasa na kuongoza majadiliano kuhusu ripoti hiyo ya maendeleo.
Aidha washiriki ambao ni wajumbe wa MUHAS HEET PIU walipata nafasi ya kuwasilisha maendeleo ya utekelezaji wa mradi kulingana na eneo husika la mradi na pia kujadili changamoto na suluhisho zinazowezekana wakati wa utekelezaji wa mradi wa HEET.
Washiriki pia waliweza kufanya kazi ya vikundi na kufanya uchambuzi wa utekelezaji wa bajeti ya 2023/24 na kuweka mpango madhubuti wa 2024/25 kulingana na makubaliano baada ya uwasilishaji wa ripoti ya maendeleo.
Katika Kikao Kazi hiki, Naibu Mratibu wa mradi wa HEET MUHAS, Dkt. Nathanael Sirili aliweza kuongoza zoezi la kuandika ombi la kuongezewa fedha ya ufadhili wa utekelezaji wa mradi huu.
Akielezea sababu kuu ya zoezi hili, Dkt Sirili alisema mpango wa awali wa utekelezaji wa mradi wa HEET kwa MUHAS ulikuwa ni kuendeleza miundombinu katika kampasi ya Upanga na ya Mloganzila. Hata hivyo, kutokana na sababu za msingi kabisa MUHAS iliagizwa kutumia theluthi moja ya bajeti iliyotengwa awali kwa ajili ya kampasi ya Upanga na Mloganzila ili kuanzisha kampasi mpya Mkoani Kigoma.
Naibu Mratibu alisisitiza kuwa fedha ya zaida itakayoombwa inalenga kuhakikisha ukamilishaji wa miundombinu iliyopangwa awali ya Ndaki ya Tiba katika kampasi ya Mloganzila na kuiwezesha kampasi ya Kigoma inayoanzishwa kuweza kufanya kazi kama inavotarajiwa.