Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amefungua rasmi Kongamano la 14 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), linalofanyika Kampasi ya Mloganzila kuanzia Julai 1–3, 2026, na kusisitiza kuwa tafiti ni msingi wa maendeleo ya elimu ya juu na kuboresha huduma za afya.
Prof. Mkenda aliipongeza MUHAS kwa mchango wake katika kuzalisha tafiti zinazosaidia kutatua changamoto za afya nchini na kueleza kuwa matokeo ya kongamano hilo yatatoa mapendekezo muhimu kwa watunga sera ili kuimarisha sekta ya afya.
Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa, alisema kongamano limewakutanisha washiriki takribani 500 kutoka ndani na nje ya nchi wanaowasilisha matokeo ya tafiti kupitia mawasilisho ya mdomo na mabango ya kisayansi. Alibainisha kuwa tafiti za chuo zimeendelea kuboresha huduma za afya, kuendeleza ubunifu na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Katika kongamano hilo, MUHAS ilisaini hati mbili za makubaliano na AUDA-NEPAD na APHRC zitakazoongeza ushirikiano katika tafiti, mafunzo, ushauri elekezi na kuimarisha vituo vya umahiri vya kikanda kwa lengo la kuzalisha ushahidi wa kisayansi unaosaidia maendeleo ya taifa.
Aidha, chuo kilizindua huduma za kisasa za Next Generation Sequencing (NGS) zitakazoboresha uchunguzi wa magonjwa, tiba binafsi, tafiti na udhibiti wa milipuko, huku zikiimarisha uwezo wa wataalamu wa ndani na kuiweka MUHAS kuwa kitovu cha kitaifa na kikanda cha huduma za jenomiki.