MUHAS NEWS POST

VIONGOZI WA MUHASSO WATEMBELEA MRADI WA UJENZI WA NDAKI YA TIBA MLOGANZILA

 

 

Viongozi wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHASSO) kimefanya ziara maalumu ya kutembelea maendeleo ya ujenzi wa Ndaki ya Tiba unaoendelea katika Kampasi ya Mloganzila ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Ziara hiyo iliratibiwa na Dkt. Hussein Mohhamed kutoka Kitengo cha Mazingira na Ustawi wa Jamii (ESIA) kupitia mradi wa HEET MUHAS ikiwa na lengo la kuwapa viongozi hao nafasi ya kujionea hatua mbalimbali za ujenzi pamoja na kuhakikisha wanafunzi wanapata taarifa sahihi kuhusu maendeleo ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa na MUHAS katika kuboresha miundombinu na utoaji wa huduma za afya nchini

Kupitia ziara hiyo viongozi wa MUHASSO walipata fursa ya kufahamu kwa undani namna miradi ya ujenzi inavyosonga mbele, ikiwemo mabweni ya kisasa, madarasa, maabara, maktaba, na maeneo ya huduma muhimu za kijamii. Pia walipata maelezo kutoka kwa mtaalamu wa ujenzi kuhusu hatua zilizokamilika na mipango iliyopo kwa hatua zinazofuata.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake mara baada ya ziara hiyo Makamu wa Rais MUHASSO, Bw. Nassir Abdulla alieleza kufurahishwa na hatua kubwa zilizopigwa na kusisitiza kuwa wanafunzi wana matumaini makubwa kuona miundombinu hii ikikamilika kwa wakati, kwani itaboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza nafasi za mafunzo kwa vitendo.

Naye Katibu Mkuu MUHASSO, Bi. Yohana Malley alisisitiza mapendekezo waliyoyatoa yafanyiwe kazi , huku akitoa shukrani kwa uongozi wa chuo na wadau wote wanaoshirikiana kuhakikisha mradi huu unatekelezwa.

Ujenzi wa Ndaki ya Tiba unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali za kupanua huduma za elimu ya juu, kuboresha miundombinu ya kufundishia na kufanya tafiti.

 

 

Facebook
Twitter
LinkedIn