Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetembelea eneo la ujenzi wa Ndaki ya Tiba katika Kampasi ya Mloganzila, ikiwa ni sehemu ya kufuatilia maendeleo ya mradi huo mkubwa wa kitaifa wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET ).
Ziara hiyo ililenga kukagua hatua zilizofikiwa, mafanikio na changamoto katika ujenzi wa majengo ya kisasa yatakayochangia kwa kiwango kikubwa katika utoaji wa mafunzo bora ya tiba na utafiti wa afya nchini.
Katika ziara hiyo, wataalamu hao walipata fursa ya kupata taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kutoka kwa wakandarasi wa kampuni ya Mohamed Builders na Hainan na kujionea jinsi ujenzi wa majengo ya kisasa unavyosonga kwa kasi, ikiwa ni pamoja na madarasa, maabara za kufundishia, Maktaba, Cafteria, bweni la wanafunzi jengo la utawala na TEHEMA vitakavyowezesha kutoa huduma bora za kitaaluma na mafunzo kwa vitendo.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, kiongozi wa timu hiyo Mhandisi Hanington Kagiraki alieleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo na aliwapongeza uongozi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kwa kushirikiana kwa karibu na wakandarasi katika kuhakikisha ubora na viwango vya ujenzi vinafuatwa ipasavyo na akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha miradi ya elimu ya juu inakamilika kwa viwango vya ubora vinavyohitajika.
Kwa upande wake Kaimu Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET MUHAS Dkt. Hussein Mohammed aliishukuru Wizara ya Elimu kwa ufuatiliaji na ushirikiano wa karibu, na kuahidi kuendelea kusimamia kikamilifu na mradi huo ili ukamilike kwa wakati uliopangwa.
Ujenzi wa Ndaki ya Tiba unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali za kupanua huduma za elimu ya juu, kuboresha miundombinu ya kufundishia na kufanya tafiti.