Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) katika utekelezaji wa maeneo saba ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya Kiuchumi (HEET) kimepokea gari la pili la aina ya Coaster kati ya magari manne yatakayo nunuliwa na mradi wa HEET kwa lengo la kurahisisha utekelezaji wa shughuli za mradi huo mkubwa ikiwemo ufuatiliaji wa masuala ya ujenzi.
Amebainisha hayo Dkt. Nathanael Sirili Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET MUHAS wakati akizungumza kwenye sherehe fupi ya kupokea gari hilo chuoni, MUHAS. Dkt. Sirili alieleza kuwa kupitia mpango wa ununuzi wa shirika la maendeleo la umoja wa mataifa (UNDP), ambao umeweza kupunguza gharama kwa kiasi kikubwa kutoka shilingi ya kitanzania milioni 450,000,000 kwa gari la kwanza na la pili hadi shilingi milioni 312,000,000/= na hivyo kuweza kuokoa takribani shilingi milioni 138 za kitanzania kama utaratibu wa kawaida ungetumika.
Dr. Sirili aliongezea kuwa gari hii itatumika kuwapeleka wafanyakazi na wanafunzi kwenye mafunzo kwa njia ya vitendo na hivyo kuimarisha mafunzo na mafungamano ya sekta ya afya na elimu kwa ujumla.
Naye Mratibu wa Mradi wa HEET MUHAS, Prof. Erasto Mbugi aliwapongeza wajumbe wa kitengo cha utekelezaji wa mradi wa HEET kwa ufanisi mkubwa katika kuhakikisha kinachopangwa ndicho kinazotekelezwa na vilevile alimshukuru Makamu Mkuu wa Chuo kwa kuhakikisha vibali vinatoka kwa kasi na kasi hiyo ndo imeleta matunda ya kupokea gari hili la pili leo.
“Gari hili linatumika katika shughuli zote cha chuo, watekelezaji wa mradi wa HEET wakiwa na shughuli watatumia nia hili ni gari la chuo ambalo limefadhiliwa na mradi wa HEET na taratibu zote za kuliendesha zitafata kama tulivyojiwekea hapa chuoni,” alisema Prof. Mbugi
Akiongea baada ya kupokea na kuzindua gari hilo, Makamu Mkuu wa Chuo, MUHAS Prof. Appolinary Kamuhabwa aliwapongeza wasimamizi wa mradi katika kufanikikisha utekelezaji wa mradi huu kwa kuleta gari la pili.
“Kikubwa hapa tumesikia tumefikisha gari la pili tukiwa tumeokoa kiasi kikubwa cha pesa na kutokana na kuokoa pesa hizo tutaweza kuongeza magari mawili mengine ambayo yatasaidia sana katika mradi na taasisi pia,”alisema Prof. Kamuhabwa.
Aidha Prof. Kamuhabwa ametoa wito kwa watekelezaji wa mradi huu kuendelea kufatilia magari mengine mawili ambayo hayajafika na kuhakikisha kuzingatia muongozo wa utunzaji wa magari haya mapya unafutatwa ikiwa lengo ni kuyalinda na kuhakikisha tunatekeleza malengo ya mradi ambao ni mahususi kwa ajili ya kuleta mageuzi ya kiuchumi katika Elimu ya juu nchini.