Katika kukabiliana na changamoto ya uhaba wa vitabu vya tiba na ugumu wa lugha kwa wanafunzi, MUHAS) kwa kushirikiana na Mhadhiri wake, Prof. David Ngasapa, wamechapisha vitabu vya anatomia ili kuboresha uelewa wa wanafunzi na kuwawezesha kufanya rejea wanapokuwa kwenye mafunzo ya kliniki.

Akizungumza na waandishi wa habari Februari 25, 2026, Prof Ngasapa alisema anatomia ni somo la msingi katika taaluma ya udaktari kwani humsaidia mwanafunzi kuelewa muundo na utendaji wa mwili wa binadamu.

Alieleza kuwa uamuzi wa kuandika vitabu hivyo umetokana na hitaji la kuwa na rejea zinazoendana na mfumo wa elimu unaolenga umahiri (Competence-Based Education), unaosisitiza uelewa na matumizi ya maarifa badala ya kukariri.

Alibainisha kuwa changamoto kubwa ilikuwa ni upatikanaji mdogo wa vitabu vya rejea, hali iliyowalazimu wanafunzi kutegemea notisi za walimu ambazo mara nyingi hutofautiana.

Aidha, vitabu vingi vilivyokuwapo viliandikwa kwa Kiingereza kigumu, hasa na waandishi ambao lugha hiyo ni ya kwanza kwao, jambo lililowapa ugumu wanafunzi wengi wa Tanzania ambako Kiingereza ni lugha ya tatu.

Prof. Ngasapa alieleza kuwa hapo awali kulikuwa na uhaba mkubwa wa vitabu vya anatomia nchini, kiasi kwamba chuoni kulikuwepo na kitabu kimoja tu ambacho wanafunzi walilazimika kunakili.

Aliongeza kuwa vitabu vipya vimeandikwa kwa lugha rahisi ya Kiingereza na vimejumuisha mifano inayoendana na mazingira ya Afrika Mashariki ili kurahisisha uelewa. Badala ya kutumia mifano ya Ulaya inayoweza kuleta mkanganyiko, vitabu hivyo vinatumia maumbo na vielelezo vinavyofahamika kwa wanafunzi wa eneo husika.

Profesa Ngasapa alisisitiza kuwa vitabu hivyo vinaendana moja kwa moja na mtaala wa sasa unaolenga umahiri, tofauti na mfumo wa zamani uliokuwa ukihamasisha kukariri.

Lengo ni kuzalisha madaktari wenye uelewa mpana wa mwili wa binadamu watakaoweza kutumia maarifa yao kwa ufanisi katika mafunzo ya klinik.

Naye, Kaimu Rasi wa Ndaki ya Tiba, Prof. Agricola Joachim, alisema wanajivunia kupata vitabu hivyo ambavyo ni muhimu kwa ajili ya kutumiwa na wanafunzi na kupata elimu wanayoihitaji.“Tunampongeza kwa kujitoa”,Alisema Prof. Joachim

 

 

 

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *