MUHAS NEWS POST

MKUU WA CHUO ATEMBELEA MUHAS

 

 

 

 

 

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof. David Mwakyusa, ametembelea MUHAS kwa lengo la kujitambulisha na kufahamiana na uongozi wa Chuo baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kushika wadhifa huo mnamo Novemba 27, 2024.

Katika ziara hiyo, Prof. Mwakyusa alipata fursa ya kukutana na Menejimenti ya MUHAS, wakiwemo Wakuu wa Shule Kuu, Rasi, Wakurugenzi, na Wakuu wa Vitengo mbalimbali, ambapo walijadili masuala muhimu kuhusu maendeleo ya Chuo.

Akimkaribisha katika kikao hicho maalum, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Appolinary Kamuhabwa, aliitambulisha rasmi Menejimenti kwa Mkuu wa Chuo na kumuelezea kuwa katika kikao hicho atapata nafasi kusikia wasilisho fupi juu ya historia ya chuo, mafanikio yaliyopatikana, miradi inayoendelea, pamoja na matarajio ya siku zijazo. Wasilisho hilo lilitolewa na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Uzamili na Uzamivu, Dr. Doreen Kamori.

Akizungumza katika kikao hicho, Prof. Mwakyusa aliipongeza Menejimenti ya Chuo kwa kazi kubwa iliyofanywa na inayoendelea kufanyika. Alisema, “Nimeona mabadiliko mengi katika mazingira ya Chuo. Hongereni kwa kazi kubwa mliyoifanya na mnayoendelea kuifanya.”

Aidha, Prof. Mwakyusa alieleza furaha yake kwa kuteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo cha MUHAS, akisema kuwa amerejea nyumbani. “Nilikuwa mwanafunzi hapa, baadaye nikawa mwalimu, na hata kushiriki katika uongozi wakati Chuo kilipokuwa sehemu ya Muhimbili Medical Centre (MMC),” aliongeza.

Katika kikao hicho, Makamu Mkuu wa Chuo alibainisha kuwa changamoto kubwa inayoikumba MUHAS katika kuendeleza shughuli zake ni upungufu wa rasilimali fedha. Alisema kuwa ruzuku inayotolewa na serikali kwa shughuli za maendeleo ya chuo ni ndogo na inaendelea kupungua, hivyo Menejimenti inajitahidi kuboresha vyanzo vya mapato ili kuendesha Chuo kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Prof. Mwakyusa alisisitiza kuwa maendeleo ya MUHAS ni jukumu la pamoja na aliahidi kushirikiana kwa karibu na Menejimenti ya Chuo, akisema kuwa yuko tayari kutoa msaada pale inapohitajika ili kuhakikisha mafanikio ya Chuo yanaendelea kupatikana.

Facebook
Twitter
LinkedIn