MUHAS NEWS POST

KATIBU MTENDAJI TCU ARIDHISHWA NA MAENDELEO YA MIUNDOMBINU YA UFUNDISHAJI NA UJIFUNZAJI MUHAS

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Charles Kihampa, ameonesha kuridhishwa na maendeleo makubwa ya miundombinu ya ufundishaji na ujifunzaji katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), huku pia akikipongeza chuo kwa juhudi zake za kuimarisha mazingira ya elimu ya juu..

Pongezi hizo zimetolewa leo, 15 Aprili 2026, wakati wa ziara ya kikazi iliyolenga kujionea hali ya miundombinu ya kitaaluma na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya chuo.

Akitoa taarifa ya taaluma, Mkurugenzi wa Masomo ya Uzamili, Prof. Doreen Kamori, alisema MUHAS kwa sasa inatoa programu 95 za uzamili, 15 za shahada ya kwanza na 7 za stashahada. Alibainisha kuwa idadi ya wanafunzi inaendelea kuongezeka na sasa imefikia zaidi ya 5,000. Aidha, chuo kina wanataaluma 447, ambapo wengi ni wahadhiri wasaidizi na wahadhiri, wanaounda takribani asilimia 20 ya jumla ya watumishi wa kitaaluma.

Kuhusu upanuzi, alieleza kuwa ujenzi wa Kampasi ya Kigoma na Ndaki ya Tiba katika kampasi ya Mloganzila unaendelea vizuri na wakandarasi wapo mbele ya ratiba, hali inayoonesha matarajio chanya ya kuanza kwa shughuli za masomo kwa wakati.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Appolinary Kamuhabwa, alieleza kuwa MUHAS inaendelea kuboresha ubora wa mitaala na kuimarisha tafiti zinazosaidia kupata ruzuku za kuendeleza shughuli za kitaaluma na kuboresha mazingira ya kujifunzia.

Prof. Kihampa alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ubora wa programu za afya ili kuhakikisha wahitimu wanakidhi viwango vya kitaifa. Wajumbe pia walipata fursa ya kutoa maoni ya kuboresha ufundishaji.

Ziara hiyo ilihitimishwa kwa kutembelea  maabara mbalimbali ikiwemo Anatomia, Patholojia, Fiziolojia, Mikrobiolojia, Biokemia, Hematolojia, Clinical Pharmacology, Anaesthesia and Clinical Care Simulation Laboratory, na Multi-User Clinical Skills Laboratory na madarasa, ambapo alijionea mazingira ya kujifunzia chuoni hapo.

 

 

 

 

 

 

Facebook
Twitter
LinkedIn