






Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimefanya Kongamano la Kisayansi la Magonjwa Adimu tarehe 4 Machi 2026 likiwa na kaulimbiu isemayo “Magonjwa Adimu: Zaidi ya Unavyoweza Kufikiria”.
Kongamano hilo limewakutanisha wataalamu wa afya, watafiti, watunga sera, wawakilishi wa wagonjwa pamoja na wadau mbalimbali kujadili changamoto na fursa zilizopo katika kushughulikia magonjwa adimu nchini Tanzania.
Akitoa salamu za ukaribisho, Kaimu Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Emmanuel Balandya alieleza kuwa kongamano hilo ni jukwaa muhimu la kitaaluma linalolenga kuimarisha mjadala, kubadilishana uzoefu na kuibua mapendekezo yatakayosaidia kuboresha utambuzi, matibabu na ubora wa maisha ya wagonjwa. Alisisitiza kuwa MUHAS ina wajibu wa kuendeleza elimu, tafiti na ubunifu katika eneo la magonjwa adimu, hasa ikizingatiwa changamoto ya upatikanaji mdogo wa vipimo vya vinasaba na gharama kubwa za uchunguzi.
Kwa upande wake, Mgeni Rasmi, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe alikipongeza chuo kwa kuandaa kongamano hilo na kuendelea kushika nafasi ya juu kitaaluma nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Alieleza kuwa licha ya kila ugonjwa adimu kuonekana kuathiri watu wachache, kwa pamoja magonjwa hayo yanaathiri mamilioni ya watu duniani, huku makadirio yakionesha kuwa asilimia kadhaa ya Watanzania wanaweza kuwa wanaishi na magonjwa hayo, wengi wao wakiwa watoto.
Alibainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuweka mikakati ya kuimarisha huduma za rufaa, kuboresha njia za huduma (care pathways), na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma jumuishi kuanzia ngazi ya msingi hadi kibingwa.
Aidha, katika kuunga mkono juhudi za utafiti na uelimishaji kuhusu magonjwa adimu, Ali Kimara Rare Diseases Foundation walitoa msaada wa hundi ya shilingi milioni mbili kwa ajili ya kusaidia kufanikisha tafiti zinazohusu masuala ya magonjwa adimu.
Msaada huo unatarajiwa kuchangia kuimarisha tafiti, kuongeza uelewa na kusaidia kuboresha huduma kwa wagonjwa wanaoishi na magonjwa hayo nchini.