Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimeingia rasmi katika awamu ya pili ya utekelezaji wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu kilichopo Mloganzila, Dar es Salaam.
Akifungua kikao cha kwanza cha Kamati ya uendeshaji ya Mradi wa awamu hii ya pili, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Prof. Nombo ambaye pia ni mwekekiti wa kamati hii alipongeza jitihada za MUHAS katika kuendeleza huduma za kitaalamu na ubunifu katika tiba na utafiti wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu. Prof. Nombo alisema kuwa hospitali mpya ya kisasa ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu itajengwa Mloganzila, karibu na jengo la awali la kituo. Hospitali hiyo itarahisisha huduma kwa wananchi, huku ikiwa ni jibu la changamoto za upungufu wa wataalamu wa upasuaji wa moyo nchini na ukanda wa Afrika chini ya jangwa la Sahara.
Aidha,Prof, Nombo aliwataka wajumbe wa kamati kushiriki kikamilifu katika kujadili masuala yote muhimu yatakayowezesha mradi kufanikisha malengo yake kwa kuzingatia thamani ya fedha na matokeo chanya katika elimu, utafiti na huduma kwa jamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki, Dkt. Rodrick Kisenge MUHAS, alifafanua kuwa awamu ya pili itahusisha ujenzi wa majengo mapya, upanuzi wa vifaa vya kisasa vya uchunguzi na tiba, pamoja na mafunzo ya kina kwa wataalamu wa afya.
Aliongeza kuwa mradi huu unaongeza nafasi ya MUHAS kuwa kitovu cha kitaifa na kikanda cha mafunzo na tiba ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.
Kituo cha Mloganzila tayari kimekuwa kiini muhimu cha kutoa huduma kwa wagonjwa, kuendesha mafunzo ya kitaalamu, na kufanya utafiti unaolenga kuboresha huduma za afya nchini. Awamu ya pili ya mradi huu inatarajiwa kuongeza uwezo wa kitengo hiki na kuhakikisha wagonjwa wengi zaidi wanapata huduma bora za matibabu na upasuaji wa moyo.