Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimepokea wageni wa heshima kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza akiwemo Mhe. Balozi Mbelwa Kairuki; Mkurugenzi Mtendaji wa Mkapa Foundation, Dkt. Ellen Mkondya; na Mkadiriaji Gharama za Majenzi kutoka Kampuni ya IP Group, Bw. Issack Peter. Wageni hao walitembelea chuo kwa lengo la kujadili fursa za uwekezaji katika ardhi ya kimkakati iliyopo kwenye Kampasi ya Mloganzila.
Katika kikao hicho cha kikazi, Prof. Gideon Kwesigapo aliwasilisha Mpango Mkuu (Master Plan) wa MUHAS unaolenga kutumia ardhi hiyo kwa miradi ya maendeleo itakayoboreshwa mazingira ya kujifunzia, kuongeza miundombinu ya kisasa, pamoja na kuimarisha huduma za afya na tafiti nchini. Alieleza kuwa uwekezaji huo utakuwa na manufaa si kwa chuo pekee bali pia kwa jamii na sekta ya afya kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mhe. Balozi Mbelwa Kairuki aliwapongeza viongozi wa MUHAS kwa jitihada za kuendeleza Kampasi ya Mloganzila na kusisitiza umuhimu wa kushirikiana na nchi rafiki pamoja na wadau wengine wa maendeleo ili kuvutia wawekezaji wabunifu wenye rasilimali na uzoefu wa kimataifa. Aidha, alishauri MUHAS kufanya ziara za kimataifa kujifunza na kuvutia fursa mpya za uwekezaji.
Dkt. Ellen Mkondya kutoka Mkapa Foundation alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha miradi inayopangwa inaleta tija ya muda mrefu kwa sekta ya afya na maendeleo ya taifa.
Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Appolinary Kamuhabwa, alisema MUHAS imepokea ushauri huo kwa moyo wa shukrani na ipo tayari kuboresha Mpango Mkuu wake ili uendane na teknolojia ya sasa. Aliongeza kuwa chuo kiko tayari kushirikiana na wawekezaji katika kuimarisha elimu ya afya, kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi, na kuliletea taifa manufaa ya kudumu.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa MUHAS wakiwemo Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Prof. Emmanuel Balandya; Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Tafiti na Ushauri wa Kiutaalamu, Prof. Bruno Sunguya; Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET, Prof. Nathanael Sirili; Prof. Gideon Kwesigapo na Bw. Geofrey Masawe kutoka Kitengo cha Biashara cha MUHAS.