Kitengo cha Mazingira na Ustawi wa Jamii (ESIA) kupitia mradi wa HEET MUHAS kimefanya mkutano na viongozi wa kata ya Kwembe iliyowajumuisha wajumbe kamati ya maendeleo, wataalamu ndani ya kata, watendaji wa mitaa, mratibu wa elimu manispaa na kata, kiongozi wa afya, wajumbe wa serikali ya mitaa, mwenyekiti wa baraza la kata na mwenyekiti wa chama CCM ili kuwapa taarifa juu ya ujio wa kambi ya kupima afya bure kwa wananchi itakayo ratibiwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili ( MUHAS) kuanzia tarehe 26 mpaka 27 februari 2025, saa tatu asubuhi mpaka saa kumi jioni katika kampasi ya Mloganzila.
Mkutano huu uliongozwa na Afisa Mtendaji wa Kata ya Kwembe, Bw. Peter Chawala ambaye alifungua mkutano kwa kuwakaribisha viongozi wote na kuishukuru timu ya MUHAS kwa kuona umuhimu wa kuja kueleza kuhusu mpango wa zoezi la upimaji wa afya bure kwa viongozi wa kata hiyo ili waweze kutoa taarifa kwa wananchi wao kushiriki kikamilifu katika kupata huduma hiyo itakayotolewa kwenye kata yao.
Akizungumza katika mkutano huu, msimamizi wa portifolio ya Ustawi wa Jamii kwenye mradi wa HEET, Prof. Emmy Metta alieleza kuwa timu ya wataalamu kutoka MUHAS imejipanga katika vitengo vyote kutoa huduma ya uchunguzi wa awali na elimu ya magonjwa mbalimbali kama macho, kinywa na meno, saratani ya matiti na shingo ya kizazi, homa ya ini, tezi dume na elimu kuhusu usugu wa madawa mwilini, lishe na magonjwa yasioambukiza.
“ Tunawapa taarifa hii ili kuwakifikishia wananchi wapate fursa ya kutumia huduma hii na tunaomba mfikishe ujumbe huu kwa wananchi walio chini yenu ili waweze kunufaika na huduma hii inayotolewa bure kwa siku mbili”, alisema Prof. Metta
Naye Diwani ya Kata ya Kwembe ,mhe.Prof. Nicholaus Lumbugo aliwashukuru timu ya MUHAS kwa kukutana na viongozi wa kata hii na kuwapa taarifa ambayo ni mpango mzuri unaoenda kusaidia wananchi kupata uchunguzi wa afya zao.
“’Naamini viongozi wenzangu yale ambayo mmeelekezwa mtaenda kutekeleza kwa ufasaha ili wananchi wa kata yetu wasipitwe na fursa hii, sisi binadamu afya ni muhimu bila afya huwezi fanya chochote”, alisema Diwani Lumbugo.
Viongozi wa kata pia walipata nafasi kupewa taarifa ya ujenzi wa majengo unaoendelea katika kampasi hiyo na kuuliza maswali, kutoa maoni na mapendekezo yao ikiwa ni pamoja na ombi la zoezi hili kuwa endelevu na kujengewa shule ya msingi katika kata yao.