Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo amefanya ziara katika Kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kilichopo Kampasi ya Mloganzila na kujionea uwekezaji mkubwa wa vifaa vya kufundishia vya kisasa na matumizi ya teknolojia ya akili mnemba (Artificial Intelligence – AI).
Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu alitembelea maeneo ya mafunzo ya magonjwa ya dharura ambapo wanafunzi na wataalamu wa afya hutumia vifaa vya kisasa kwa mafunzo ya vitendo. Vifaa hivyo vimeundwa mahsusi kusaidia kujifunza mbinu za haraka za kuokoa maisha, sambamba na teknolojia ya akili mnemba inayorahisisha ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa muhimu kwa ajili ya huduma na tafiti za kiafya nchini.
Katibu Mkuu amepongeza jitihada za kituo hicho kwa kuendelea kuimarisha elimu ya kitabibu kupitia matumizi ya teknolojia ya akili mnembe (Artificial Intelligence), inayotumika kurahisisha ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu za kiafya pamoja na kufanikisha mafunzo kwa wanafunzi na wataalamu wa afya.
Ameeleza kuwa matumizi ya vifaa hivyo na AI yanachangia sio tu katika kuongeza ufanisi wa utoaji wa elimu ya kitabibu, bali pia katika kusaidia taifa kupata takwimu sahihi za kiafya zitakazowezesha kuboresha sera na mipango ya afya nchini.
Aidha, Katibu Mkuu ameongeza kuwa uwepo wa teknolojia hiyo katika kituo cha umahiri cha Mloganzila ni kielelezo cha mabadiliko chanya katika sekta ya elimu na afya, hasa kupitia miradi mikubwa ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.
“Teknolojia ya akili mnembe inatoa nafasi ya wanafunzi na wataalamu kujifunza kwa vitendo, kwa uhalisia zaidi, na pia kutengeneza mifumo ya kitaifa ya takwimu za magonjwa. Hii ni hatua kubwa katika mageuzi ya elimu na huduma za afya,” amesema Katibu Mkuu.
Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu Mloganzila ni sehemu ya jitihada za kitaifa kuhakikisha Tanzania inakuwa na wataalamu bingwa wa afya wanaotumia teknolojia za kisasa katika kutoa huduma bora, sambamba na kufanya tafiti zenye mchango mkubwa katika ustawi wa wananchi.