Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) katika utekelezaji wa maeneo saba ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya Kiuchumi (HEET) kimepokea gari la kwanza la aina ya Land Cruiser Hardtop kati ya magari manne yatakayo nunuliwa na mradi wa HEET kwa lengo la kurahisisha utekelezaji wa shughuli za mradi huo mkubwa ikiwemo ufuatiliaji wa masuala ya ujenzi.
Amebainisha hayo Dkt. Nathanael Sirili Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET MUHAS wakati akizungumza kwenye sherehe fupi ya kupokea gari hilo chuoni, MUHAS. Dkt. Sirili alieleza kuwa kupitia mpango wa ununuzi wa shirika la maendeleo la umoja wa mataifa (UNDP), gari hili limegharimu takribani shilingi za kitanzania 165,000,000/= na hivyo kuweza kuokoa takribani shilingi milioni 100 za kitanzania kama utaratibu wa kawaida ungetumika.
Naye Mratibu wa Mradi wa HEET MUHAS, Prof. Erasto Mbugi aliwapongeza wajumbe wa kitengo cha utekelezaji wa mradi wa HEET kwa ufanisi mkubwa katika shughuli mbalimbali za mradi ambao umewezesha kupata matunda ya kazi wanazofanya.
“Moja ya majukumu ya utekelezaji wa mradi wa HEET ni pamoja na ununuzi wa vitendea kazi, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa gari ambalo tunalipokea leo. Gari hili ni mahususi kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za mradi,” alisema Prof. Mbugi
Akiongea baada ya kupokea na kuzindua gari hilo, Makamu Mkuu wa Chuo, MUHAS Prof. Appolinary Kamuhabwa aliwapongeza wasimamizi wa mradi katika kufanikikisha utekelezaji wa mradi huu na akasema hatua ya leo inaashiria mradi unaendelea vizuri.
“Kwa maeneo mengine ya mradi kama vile kwa upande wa mitaala tuko mbele ukilinganisha na taasisi nyingine na kwa upande wa ujenzi wa kampasi ya Mloganzila tunategemea mwazoni wa Novemba mkandarasi ataanza kazi na kwa upande wa kampasi ya Kigoma tunategemea mwezi huo huo wa Novemba mkandarasi atakuwa amepatikana, kwa hiyo hivi vitendea kazi vitaenda kutumika katika kusaidia kazi hiyo”, alisema Prof. Kamuhabwa.
Aidha Prof. Kamuhabwa ametoa wito kwa watekelezaji wa mradi huu kuendelea kushirikiana ili kuweza kutekeleza malengo ya mradi ambao ni mahususi kwa ajili ya kuleta mageuzi ya kiuchumi katika Elimu ya juu nchini.