Mkurugenzi wa Masomo ya Uzamili wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof. Doreen Kamori, amefunga rasmi mafunzo ya usafishaji damu (Hemodialysis) yaliyodumu kwa wiki sita, huku akiwapongeza waandaaji na washiriki kwa kujitolea kuimarisha huduma za afya nchini.
Prof. Kamori amesema washiriki 31, wakiwemo madaktari na wauguzi kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Arusha, Manyara, Morogoro, Kilimanjaro, Singida, Dar es Salaam na Zanzibar walijiandikisha katika mafunzo hayo, ambapo wahitimu 29 wamefanikiwa kukamilisha
programu hiyo.
Amesema mafunzo hayo yalihusisha wiki moja ya darasani na wiki tano za mafunzo kwa vitendo katika vituo vya huduma za dialysis vya Hospitali ya Taifa Muhimbili na African Health Network.
Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo, Prof. Kamori amesema huduma za dialysis zina umuhimu mkubwa kutokana na ongezeko la wagonjwa wa figo nchini na duniani, akibainisha kuwa takwimu zinaonyesha watu 7 hadi 15 kati ya kila watu 100 nchini Tanzania wana
changamoto za figo, huku zaidi ya wagonjwa 4,000 wakipatiwa huduma za dialysis nchini kwa sasa.
Aidha, amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuboresha huduma hizo kwa kuongeza vituo vya dialysis katika hospitali za mikoa, huku akisisitiza kuwa upatikanaji wa wataalamu wenye ujuzi ni msingi muhimu wa utoaji wa huduma bora na salama.
Amewataka wahitimu kutumia maarifa waliyojifunza kuboresha huduma katika vituo vyao vya kazi, kuendeleza weledi wa kitaaluma pamoja na kuwafundisha wataalamu wengine ili kuimarisha zaidi huduma kwa wagonjwa wa figo nchini.
Prof. Kamori pia amewapongeza waandaaji wa mafunzo hayo na kueleza matarajio ya kuona awamu nyingine ya mafunzo ikitangazwa mapema ili kuwafikia wataalamu wengi zaidi.