Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wamesaini makubaliano ya ushirikiano yatakayolenga kuimarisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote kupitia tafiti, uchambuzi wa takwimu, mafunzo
pamoja na kujenga uwezo kwa wataalamu na wanafunzi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa, aliishukuru NHIF kwa ushirikiano mkubwa ambao tayari umejengwa kati ya taasisi hizo, hususan kupitia Shule Kuu ya Kinywa na Meno ya MUHAS, ambapo huduma za kliniki zimeendelea kuimarika na kutoa manufaa kwa jamii.
Prof. Kamuhabwa alisema makubaliano hayo yanaendana na dhamira ya chuo ya kuendeleza programu za afya zinazounga mkono vipaumbele vya taifa kupitia ushirikiano wa karibu na Wizara ya Afya.
“Tunatarajia kuanzisha programu mbalimbali zitakazosaidia utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote. MUHAS ina wataalamu wa kufanya uchambuzi wa takwimu, mifumo ya kisasa ya uchakataji wa taarifa pamoja na uwezo wa kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha huduma za afya nchini,” alisema Prof. Kamuhabwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dkt. Irene Isaka, alisema ushirikiano huo utakuwa muhimu katika kuimarisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote kupitia tafiti, uchambuzi wa taarifa na ushahidi wa kisayansi
utakaosaidia kufanya maamuzi sahihi ya kisera na kiutendaji.
Aliongeza kuwa matokeo ya tafiti zitakazofanyika pia yatasaidia kujenga uwezo kwa watumishi pamoja na wanafunzi wanaopata mafunzo katika sekta ya afya.
Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Prof. Emmanuel Balandya, alisema chuo kina matarajio makubwa kupitia ushirikiano huo, hususan katika eneo la mafunzo kwa kuandaa mitaala itakayosaidia kuongeza ujuzi na kujenga uwezo kwa wanafunzi.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Tafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Prof. Bruno Sunguya, alisema MUHAS inaongoza katika kufanya tafiti zenye ushahidi wa kisayansi na ina wataalamu wa kutosha katika maeneo ya uchumi wa afya na
mifumo ya afya.
Aliongeza kuwa chuo kimeendelea kunufaika kupitia ushirikiano wake na taasisi mbalimbali, huku akisisitiza kuwa kila ushirikiano una mchango muhimu katika kuleta maendeleo ya kitaaluma na kitaifa.
Aidha, MUHAS ilipongezwa kwa hatua zake za kuhamasisha na kusajili wanafunzi katika huduma za bima ya afya, jambo ambalo limeiwezesha kufanya vizuri ikilinganishwa na baadhi ya taasisi nyingine za elimu ya juu nchini.