



















Machi 8 ni siku ya Wanawake Duniani na siku ambayo dunia inathamini na inaungana pamoja katika kutambua na kupongeza mafanikio ya wanawake na hasa katika maendeleo ya uchumi. MUHAS kupitia kitengo cha jinsia waliandaa hafla maalum kwa ajili ya wafanyakazi wanawake katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani hapa chuoni.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mkuu wa Kitengo cha Jinsia Dkt. Hawa Mbawala alitoa shukrani za dhati kwa uongozi wa MUHAS kwa kutambua uwepo na kujali michango ya wafanyakazi wanawake MUHAS.
Akielezea baadhi ya mafanikio yaliofanywa na uongozi wa MUHAS katika maswala ya jinsia ni kuwa na kitengo cha jinsia na kamati yake, uwakilishi wa kitengo cha jinsia katika vyombo vya maamuzi ya Chuo, kuwa na sera ya jinsia na kupinga ukatili na ubaguzi na usawa wa kijinsia kuwa moja ya malengo makuu ya kiutendaji hapa chuoni.
Dkt Mbawala alisisitiza kwa kusema “Taasisi yetu inathamini sana wanawake, kwa kulingana na kauli mbiu ya mwaka huuKizazi cha Haki na Usawa Kwa Maendeleo Endelevu suala hili limepewa kipaumbele kulingana na hatua zilizofanya na Chuo chetu”. Alizidi kufafanua kuwa kitengo cha jinsia ni mnufaika katika Mradi wa HEET ambao utasaidia kujenga uwezo kwa wafanyakazi, miundombinu, kupata mafunzo na kuimarisha njia za kuripori ili kutokomeza ukatili wa kijinsia hapa Chuoni.
“Vilevile Chuo kinatupa bajeti ya kila mwaka kwa ajili ya kuendesha mafunzo ya uelewa na udhibiti ya ukatili wa kijinsia, kufanya semina za muongozo kazi kwa wanafunzi wetu wa kike ili kupata wanataaluma na watafiti na vile vile tunafanya semina na watoto wakike katika shule za sekondari ili kuongeza udahili”.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi, Muhimbili, Prof. Andrea Pembe aliwapongeza waratibu wa jinsia kwa kuwa na kauli mbiu mahususi ya MUHAS isemayo Usawa wa Kijinsia Kwa Maendeleo Eendelevu Katika Mafunzo na Tafiti Katika Fani za Afya ambayo ina ujumbe maalum ndani ya taasisi na nchi yetu.
Akizungumzia changamoto kwenye upande wa usawa na jinsia Prof. Pembe alisema kuwa kwa miaka ya nyuma kwenye fani ya udaktari, katika madaktari hamsini (50) wanaodahiliwa, kumi (10) walikuwa wanawake ambayo ni kama asilimia ishirini (20%). “Leo hii tunazungumzia asilimia arobaini (40%) ya wanafunzi tunao wadahili hapa chuoni kwetu ni wasichana, ila bado tunahitaji kuwajengea mazingira watoto wetu wa kike ili waweze kupata elimu na kuwahamasisha wasome masomo ya sayansi”, aliongeza. Prof Pembe alieleza kwamba hili linawezekana kwa kuwaonyesha watoto hawa wa kike ushuhuda wa watu ambao wamesoma masomo ya sayansi na kupata maendeleo ili tunaweza kuwafikisha wanapotaka na hivyo kutaongeza idadi ya watoto wa kike wanaaodahiliwa hapa Chuoni.
Katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Wanawake wa MUHAS walipata fursa ya kusikia shuhuda mbalimbali kuhusiana na maisha ya baadhi ya wanawake walifanya kazi MUHAS kwa zaidi ya miaka 25. Kutoka kwa wanawake wataalamuma Prof. Sheila Maregesi kutoka Shule ya Famasia na kwa upande wa wanawake waendeshaji Bi Ritha Sindika, Katibu Muhtasi kwenye Ofisi ya Naibu Makamu wa Chuo, Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaaluma walielezea ushuhuda wao na kutoa nasaha kwa wanawake wa MUHAS. Vile Vile wanawake wa MUHAS walijumuika na uongozi wa Chuo kwa kupata chakula cha mchana kwa pamoja hapa Chuoni.