





Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, MUHAS kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi, HEET leo kimefanya makabidhiano ya eneo (site) na Mshauri wa masuala ya mazingira kwa ajili ya kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Kijamii, ESIA katika maandalizi ya ujenzi wa Ndaki ya Tiba katika Kampasi ya Mloganzila
Akizungumza katika kikao cha awali kati ya wajumbe wa Kitengo cha Utekelezaji wa Mradi, PIU MUHAS na timu ya Mshauri wa masuala ya mazingira kutoka Eco Service Limited in association with Kaskim Company Limited, Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi MUHAS, Bw, Charles Mnyeti amesema kuwa madhumuni ya kikao hiki ni kutambuana na kuwa na uelewa wa pamoja katika kazi inayokwenda kufanyika kupitia mradi huu.
Akizungumza katika Kikao hiki, Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET MUHAS, Dkt. Nathanael Sirili ameeleza kuwa hatua hii ni muhimu sana katika utekelezaji wa mradi hasa katika upande wa ujenzi wa miundombinu ya kufundishia katika Kampasi ya Mloganzila. Amesema kuwa kazi ambayo wanakwenda kuifanya itawezesha kazi nyingine kubwa kuweza kuanza kufanyika,
Naibu Mratibu amesisitiza kuwa hatua zinazofuata kwa ajili ya ujenzi wa Ndaki ya Tiba zinategemea kukamilika kwa kazi hii na hivyo akamsihi mshauri kuangalia uwezekano wa kupunguza muda wa kuimaliza bila kuathiri ubora wa kazi. Amesema ni muhimu kuhakiksha kazi inafanyika kwa ukamilifu wake.
Akizungumzia Mradi wa HEET, Dkt. Sirili amesema ni mradi wa elimu ya juu unaofadhiliwa na serikali kupitia fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia na kuratibiwa kitaifa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Ameongeza kuwa kufanya kazi hii kwa umakini ni nafasi pia ya kuchangia katika maendeleo na mageuzi ya uchumi katika sekta ya elimu ya juu nchini.
Katika Kikao hiki, msimamizi wa mazingira wa mradi wa HEET MUHAS, Dkt Hussein Mohamed alitambulishwa kama Meneja wa Mkataba wa ESIA na akawapitisha wajumbe kwenye hadidu rejea za mkataba. Dr. Mohamed alisisitiza kwamba kazi inayokwenda kufanyika ni matakwa ya kisheria ambayo inataka kabla ya kufanyika maendeleo yoyote kama MUHAS inayotaka kuyafanya katika Kampasi ya Mloganzila ni lazima ESIA ifanyike.
Naye Mkurugenzi wa Kaskim Company Limited, Ms Regina Kabwogi aliahidi kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na kuomba ushirikiano wa karibu na haraka pale utakapohitajika ili kuweza kukamilisha kazi hii mapema iwezekanavyo.