skip to Main Content
P.O. Box 65001, MUHAS,Dar es Salaam webmaster@muhas.ac.tz 0752360543 / 0756265177 - Admission Office
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Appolinary Kamuhabwa akitoa taarifa kuhusu mpango wa motisha wa chuo wakati wa mkutano na watumishi wa MUHAS
Watumishi wa MUHAS wakifatilia taarifa inayotolewa na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo wakati wa mkutano uliyofanyika chuoni, MUHAS
Watumishi wa MUHAS wakifatilia taarifa inayotolewa na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo wakati wa mkutano uliyofanyika chuoni, MUHAS
Bw. Omary Killo akiuliza swali kwa Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo baada ya kupokea taarifa wakati wa mkutano.
Bw. Charles Marwa akiuliza swali kwa Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo baada ya kupokea taarifa wakati wa mkutano.
Kaimu Makamu Mkuu wa chuo akiwa kwenye picha ya pamoja na Manaibu Makamu na watumishi waendeshaji wa MUHAS mara baada ya mkutano uliyofanyika chuoni hapo
Kaimu Makamu Mkuu wa chuo akiwa kwenye picha ya pamoja na Manaibu Makamu na watumishi wanataaluma wa MUHAS mara baada ya mkutano uliyofanyika chuoni hapo

31 Agosti, 2023

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Appolinary Kamuhabwa leo amekutana na watumishi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, MUHAS kwa lengo la kutoa taarifa na kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya Chuo.

Akizungumza katika Kikao hiki, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo amesema, ajenda kuu ya kikao ni kuwapa taarifa kuwa Mpango wa Motisha wa Chuo umeidhinishwa kama ulivyowasilishwa Serikalini ili uweze kuanza kutumika.

Akifafanua zaidi, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo amesema japokuwa Mpango umepitishwa lakini mpango huu haupo katika bajeti ya mwaka 2023/2024 kwa hiyo hauwezi kutekelezwa kama ulivyo. Hata hivyo, alieleza kuwa Menejimenti ya Chuo ilikaa na kuangalia kama kuna kipengele ambacho kinagusa watumishi wote na kinaweza kuanza kutekelezwa bila kuathiri bajeti ya Chuo.

Baada ya kufanya tathmini hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo alisema, uongozi ulijiridhisha kuwa kipengele cha posho ya nyumba kwa watumishi kinaweza kuanza kutolewa kuanzia mwezi Septemba 2023. Gharama ya posho ya nyumba ni asimilia 69 ya fedha yote ya mpango wa motisha. Prof. Kamuhabwa alisisitiza kuwa viwango vitakavyotolewa ni vile vilivyoainishwa kwa kila kada kwenye Mpango huu na kuidhinishwa na Serikali.  

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo pia alieleza kuwa watumishi wanataaluma kuanzia ngazi ya mhadhiri mwandamizi na watumishi wenye nafasi za uongozi na watumishi ambao ni madaktari wa binadamu na madaktari wa kinywa na meno wataendelea kupata posho ya nyumba kutoka Serikalini na Chuoni kama awali kwa mujibu wa sheria. Ameongeza kuwa mpango wa motisha wa Chuo umeangalia watumishi wengine wote ambao hawana haki ya kisheria ya kupewa posho ya nyumba ili nao waweze kunufaika na posho hii.

Akifafanua zaidi, Prof. Kamuhabwa amesema gharama ya utekelezaji wa mpango huu wa motisha inatokana na mapato ya ndani ya Chuo na tathmini iliyofanyika wakati mpango unaandaliwa inaonyesha kuwa asimilia 10 ya mapato ya ndani yatatumika kugharamia mpango huu ambayo ni takribani kama bilioni 1.1 kwa mwaka.

Hivyo, Prof. Kamuhabwa amesisitiza umuhimu wa kuwa na mpango mkakati wa kuzalisha fedha ili kuweza kuutekeleza mpango huu kikamilifu. Kwa kuzingatia hilo Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo ameunda kamati ya wataalam ambayo itasaidiana na Mkurugenzi wa Mipango, Maendeleo na Uwekezaji kutengeneza mpango mkakati huu. “Kadiri tutakavyozalisha fedha ndivyo tutakavyopata nguvu za kuutekeleza mpango huu lakini vile vile kuweza kuboresha baadhi ya viwango vilivyopo,” aliongeza.

Katika Kikao hiki, Makamu Mkuu wa Chuo pia alizungumzia jitihada za kuboresha hali ya usafi Chuoni na kusema ameunda kamati ya mazingira ambayo inaongozwa na Dkt Hussein Mohamed, Mtaalam wa mazingira kutoka Shule Kuu ya Afya na Sayansi za Jamii. Kamati hii itapita kwa watumishi ili kuweza kupata mawazo, ushauri na maoni ili kuweza kuboresha mazingira ya MUHAS.

Prof. Kamuhabwa pia amezungumzia changamoto la uhaba wa ofisi na vyumba vya madarasa na kuelezea mpango uliopo wa kuwa jengo ambalo litakuwa na ofisi za watumishi na vyumba vya madarasa. Amesema kamati ndogo imeundwa kushughulikia hilo ambayo inaongozwa na Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taalluma, Prof. Emmanuel Balandya. Kamati hii pia ina wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi ambao wanaendelea na michoro na pia itaainisha eneo la kujenga hili jengo.

Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi – HEET (Higher Education for Economic Transformation Project) ulikuwa ni moja ya ajenda katika Kikao hiki. Prof. Kamuhabwa alisema kuwa mradi huu unafadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Serikali ya Tanzania na MUHAS ikiwa ni miongoni mwa wanufaika wa takribani dola za kimarekani milioni 45. Fedha hizi kwa kiasi kikubwa zitajenga Kampasi ya Mloganzila na Kampasi ya Kigoma.

Katika Kikao hiki watumishi pia walipata nafasi ya kuuliza maswali, kutoa maoni na mapendekezo ya kuboresha ustawi wa Chuo na watumishi kwa ujumla. Pia watumishi walipongeza na kuishukuru menejimenti kwa hatua hii ya utekelezaji wa mpango wa motisha kwenye kipengele cha posho ya nyumba.