



Dr. Rehema Chande akielezea mchakato mzima wa kukusanya na kuandaa data kwa ajili uanishaji wa ubora wa Vyuo Vikuu unaofanywa na mtandao wa kimataifa wa Times Higher Education (THE)


Tarehe 25 Agosti, 2023
Uongozi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), leo umewapongeza Prof. Eligius Lyamuya na Dr. Rehema C. Mallya kwa uongozi wao mahiri kwenye zoezi la kuandaa na kuwasilisha data kwenye mtandao wa kimataifa wa Times Higher Education (THE) na hivyo kuiwezesha MUHAS kuwa miongoni mwa Vyuo Vikuu vitatu bora katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Akizungumza katika hafla hii ya kuwapongeza, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Appolinary Kamuhabwa amewashukuru viongozi hawa kwa kazi kubwa waliyoifanya ambayo matokeo yake yameweza kukipatia Chuo sifa kubwa ndani na nje ya nchi. Pia amempongeza na kumshukuru Prof. Lyamuya kwa kuendelea kuwa mshauri (mentor) mzuri hapa Chuoni kwenye masuala la taaluma na masuala ya uongozi
Aidha Prof Kamuhabwa amewaomba wakuu wa ndaki, shule kuu, kurugenzi, idara na vitengo mbalimbali Chuoni watoe ushirikiano wa karibu na haraka pale data zitakapohitajika tena kwa ajili uanishaji wa ubora wa Vyuo Vikuu utakaofuata. Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo pia amesisitiza umuhimu wa usahihi wa taarifa zinazowasilishwa kwa ajili ya uanishaji wa ubora.