

Wajumbe wa Kitengo cha Utekelezaji wa Mradi wa HEET MUHAS wakiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Appolinary Kamuhabwa






Kitengo cha utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) cha Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimefanya Kikao Kazi cha siku tano kupitia utekelezaji wa mradi kwa mwaka 2022/2023 na kutengeneza Mpango Kazi wa mwaka 2023/2024.
Naibu Mratibu wa Kitengo ya Utekelezaji wa Mradi wa HEET MUHAS, Dr. Nathaniel Sirili ameeleza kuwa dhumuni la Kikao Kazi hiki ni kupitia malengo ya mpango mazi uliopita na kujadili kwa pamoja mafanikio yaliyopatikana, changamoto za utekelezaji na nini kifanyike kwenye mpango kazi wa mwaka huu kufanikisha utekelezaji.
Akiwasilisha mpango kazi kwa mwaka huu kwa Kaimu Makamu wa Chuo, Mwenyekiti wa Kikao Kazi ambaye pia ni Msimamizi wa Ufuatiliaji na Utathmini wa Mradi, Dr. George Ruhago amesema kuwa mpango kazi uliomalizika umekuwa na mafanikio makubwa kwenye baadhi ya maeneo ambayo mwanzoni yalikuwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na eneo la mafunzo na eneo manunuzi.
Dr. Ruhago aliongeza kuwa mafanikio pia yameonekana kwenye uelewa wa mradi kwa wajumbe wa Kitengo cha Utekelezaji wa Mradi (Project Implementation Unit – PIU). Amesema kuwa mwanzoni uelewa wa mradi kwa wajumbe haukuwa wa pamoja lakini sasa uelewa umeongezeka na wajumbe wameanza kuona kwamba hakuna eneo la mradi liko peke yake bali kila kitu kinashirikiana.
Akizungumza na wajumbe wa Kikao Kazi hicho, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Appolinary Kamuhabwa aliwashukuru kwa kujitoa kwao kutekeleza mradi huu wa kitaifa na kuwasisitizia kuwa wameaminiwa kubeba dhamana ya MUHAS kwenye mradi huu.
Prof. Kamuhabwa amesema kuwa japokuwa mradi uko nyuma kwa zaidi ya mwaka mmoja kutokana na sababu mbalimbali za msingi, ikiwa ni pamoja ya mabadiliko wa waratibu wa mradi wawili mfululizo ambao walipata nyadhifa nyingine nje ya Chuo, mradi sasa unaenda vizuri. Amewapongeza wajumbe wote kwa juhudi kubwa zilizofanyika kwa kipindi kifupi ambapo mafanikio yameanza kuonekana.
Akisisitiza umuhimu wa mradi huu kwa Chuo na Taifa kwa ujumla, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo amesema, ajenda ya utekelezaji wa mradi wa HEET imepelekwa kwenye Baraza la Chuo ambalo ni ndio chombo cha juu kabisa kinachosimamia uendeshaji wa taasisi, na itakuwa ni ajenda ya kudumu.
Prof. Kamuhabwa alisema japokuwa Baraza la Chuo lilikuwa na wasiwasi kwamba mradi unaenda kukwama kutokana taarifa mbalimbali walizokuwa wanazipata huko mwanzo, wajumbe walifurahishwa na kuridhika na wasilisho la utekelezaji wa mradi wa HEET lililofanywa kwenye kikao cha Baraza tarehe 8 Agosti, 2023. “Kuna matumani makubwa kwa juhudi ambazo mnazifanya na sisi kama menejimenti tutahakikisha kwamba tunawezesha zile shughuli zenu”, aliongeza.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo pia alipongeza utaratibu huu wa kuwa na kikao kazi cha kupitia mpango kazi uliopita umefanyikaje, umefanikiwa wapi, mapungufu yake ni yapi na nini kifanyike kwenye mpango kazi wa mwaka unaokuja.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuwashirikisha wadau hasa wa ndani kwa kutumia vikao mbalimbali ili kusudi watu wote wauelewe mradi na wauone ni mradi wetu sote kama jumuiya ya MUHAS na sio wa watu wachache ambao wamepewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa mradi huu.
Kikao kazi hiki kimefanyika tarehe 14 – 18 Agosti, 2023, Morogoro na kuhudhuriwa na wajumbe wa Kitengo cha Utekelezaji wa Mradi wa HEET MUHAS. Wajumbe PIU pia walipata nafasi ya kuweza kutembelea eneo la MUHAS lililopo Kihonda Morogoro.