







27 Julai, 2023
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesisitiza uwazi na haki kama kigezo muhimu kwenye Samia Scholarship.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, MUHAS kutangaza fursa ya Samia Scholarship, Waziri alifafanua kuwa haki ni kwa yule ambaye amefaulu vizuri zaidi ndio atakayenufaika na ufadhili huu na hakuna kigezo kingine.
Akitoa ufafanuzi zaidi wa ufadhili huu, Prof. Mkenda alisema Samia Scholarship ilianzishwa 2022/2023 na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ufadhili huu uliwalenga wanafunzi wanaohitimu Kidato cha Sita wenye ufaulu wa juu katika tahasusi za sayansi (PCB, PCM, PGM, CBG, CBA, PMC na CBN) kupata udahili katika fani za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Tiba kwenye vyuo vya Elimu ya Juu nchini.
Prof Mkenda alieleza kuwa lengo la ufadhili huu ni kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya sayansi ili hatimaye taifa lipate rasilimali watu wa kutosha kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya nchi na watu wake.
Akitoa taarifa ya ufadhili huo kwa mwaka wa 2023/2024, Waziri alisema Serikali imetenga jumla ya TZS 6.7 bilioni kugharimia wahitimu wa Kidato cha Sita wapatao 640 watakaonufaika Samia Scholarship. Aliongeza kuwa wanufaika wa ufadhili huu watawajibika kuzingatia masharti ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kiwango cha ufaulu wao hakipungui GPA 3.8 katika mwaka wa masomo.
Katika mkutano huu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo alitoa mchanganuo wa Samia Scholarship kwa mwaka 2022/2023, na kusema kuwa jumla ya wanafunzi 636 walinufaika na ufadhili huu na kudahiliwa na kusajiliwa katika taasisi 18 za Elimu ya Juu nchini, za kiserikali na zisizo za kiserikali.
Prof. Carolyne Nombo aliongeza kuwa idadi kubwa ya wanufaika walikwenda katika vyuo vikuu ambavyo vinatoa taaluma za tiba ikiwemo MUHAS ambao waliweza kupata wanufaika 232 ni kama asilimia 36 ya wanufaika wote wa Samia Scholarship. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa sababu ya uwingi wa program walizonazo ambazo zinapata ufadhili walikuwa na jumla ya wanafunzi 311 ambayo ni kama asilimia 48, alieleza.
Katibu Mkuu alifafanua kuwa Samia Scholarship inagharamia kwa asilimia mia moja (100%) masomo ya Chuo Kikuu kwa wanafunzi ambao wamepata udahili katika fani za Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Tiba. Ufadhili utazingatia viwango na miongozo ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu na utagharamia ada ya mafunzo, posho ya chakula na malazi, posho ya vitabu na viandikwa, mahitaji maalum ya vitivo, mafunzo kwa vitendo, utafiti, vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na bima ya afya.
Katika Mkutano huu, baadhi ya wanufaika wa Samia Scholarship kutoka MUHAS walipata nafasi ya kutoa shukrani kwa Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ufadhili huu. Walisema kuwa ufadhili huo unachochoa juhudi zaidi ili wasipoteze fursa hii na pia imekuwa ni chachu kwa walio nyuma yao kuongeza bidii zaidi katika masomo na kuweza kupata fursa hiyo.
Naye Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, MUHAS, Prof. Emmanuel Balandya akitoa salamu za ukaribisho alishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuona umuhimu wa kuwa na hii scholarship ambayo imekuwa ya manufaa na msaada mkubwa kwa wanafunzi wengi wa MUHAS. Prof. Balandya pia amemshukuru Waziri kwa kukipa heshima Chuo kwa kuamua kufanyia Mkutano huu hapa MUHAS.
Awali akizungumza na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Waziri alisema ameamua kufanya mkutano huu MUHAS ili kuwapongeza na kuwapa moyo kutokana na kutangazwa hivi karibuni kama Chuo Kikuu bora nchini na cha tatu Kusini mwa Jangwa la Sahara.