skip to Main Content
P.O. Box 65001, MUHAS,Dar es Salaam webmaster@muhas.ac.tz 0752360543 / 0756265177 - Admission Office
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye akiongea kwenye kikao na timu ya wajumbe wa Kamati ya uratibu wa mradi wa HEET MUHAS pamoja na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Kigoma
Wajumbe wa Kamati ya Uratibu wa mradi HEET MUHAS na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Kigoma wakiwa katika kikao maalum kujadili  mipango na mikakati ya kuanzisha Kampasi ya MUHAS Kigoma.
Wajumbe wa Kamati ya Uratibu wa mradi HEET MUHAS na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Kigoma wakiwa katika kikao maalum kujadili  mipango na mikakati ya kuanzisha Kampasi ya MUHAS Kigoma.
Mwakilishi, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mjumbe wa Kamati ya Uratibu wa Mradi wa HEET Kitaifa, Dr. Rehema Holela, akitoa salamu za Wizara
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Utafiti na ushauri wa kitaalamu, Prof. Bruno Sunguya akitoa salamu za MUHAS
Mratibu wa mradi HEET MUHAS, Prof. Erasto Mbugi akitoa salamu za utangulizi na utambulisho wa timu kutoka MUHAS
Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET MUHAS Dr. Nathanaeli Sirili akitoa wasilisho kuhusu uanzishwaji wa Kampasi ya Kigoma

28 Juni, 2023

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye ameahidi ushirikiano kamili kutoka katika mkoa wake ili kurahisisha utekelezaji wa ujenzi Kampasi ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Kigoma chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).

Akizungumza kwenye kikao na timu ya wajumbe wa Kamati ya uratibu wa mradi wa HEET MUHAS pamoja na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Kigoma, kujadili mikakati na mipango mbalimbali ya kuanzisha Kampasi ya MUHAS Kigoma, RC Andengenye amesema hakuna taasisi ya serikali ambayo itakwamisha mradi huu ndio maana amawaita wote kwenye kikao hiki.

Amesema kuwa kama mkoa wa Kigoma wamelipokea hili jambo kwa furaha kubwa na kutoa uhakika kwamba kila mmoja kwa nafasi yake atatekeleza kile kinachohitajika ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huu.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Utafiti na ushauri wa kitaalamu, Prof. Bruno Sunguya amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuitikia wito wa kikao hiki na kuwaleta wadau mbalimbali na viongozi wa serikali wa Kigoma. Amesisitiza kuna muda mfupi umebaki wa utekelezaji wa mradi takribani miaka miwili na nusu na endapo kila mtu akifanya kwa nafasi yake tutaweza kukamilisha kwa wakati.

Akitoa salamu za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Rehema Horera alielezea kwa kifupi mradi wa HEET na kusema ni mradi wa elimu ya juu unaofadhiliwa na serikali kupitia fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia na kuratibiwa kitaifa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Alisema mradi unatekelezwa na vyuo vikuu vyote vya umma nchini kutokana na mahitaji yaliyopo na MUHAS ni mmoja wa wanufaika.

Katika Kikao hiki Mratibu wa HEET MUHAS ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Erasto Mbugi amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuipatia MUHAS ardhi kwa ajili ya ujenzi wa Kampasi hii pamoja na ofisi kwa ajili ya uratibu wa shughuli zote za mradi.

Amesema kuwa hii ni alama wazi kuwa Mkoa wa Kigoma uko mbele katika kutekeleza kwa vitendo maono ya Rais wa Awamu ya sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kusogeza na kuboresha huduma kwa wananchi.

Naye Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET MUHAS Dkt Nathaniel Sirili akiwasilisha wasilisho kuhusu uanzishwaji wa Kampasi ya Kigoma alieleza kuwa ili kushughulikia upungufu wa wataalam wa afya nchini, Serikali inaanzisha kampasi ya MUHAS, Kigoma na jumla ya dola za kimarekali milioni 15 (takriban bilioni 36 za kitanzania) zimetengwa kwa ajili hiyo.

Akizungumzia baadhi ya faida za uwepo wa Kampasi ya MUHAS Kigoma, Dkt Sirili amesema utapelekea kutumika kwa hospital za mkoa huu na Jirani katika utoaji wa mafunzo kwa vitendo na hivyo kufanya wataalam wa afya bobezi kutoka MUHAS kushiriki mojamoja katika utoaji wa huduma. Amesema pia utachochea ujenzi wa hospital kubwa kwa ajili ya kufundishia na hivyo kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma za Kibingwa mkoani Kigoma.

Katika kikao hiki Mwenyekiti wa Kamati ya Hisnia ya MUHAS (Industrial Advisory Committee), Dkt Mary Mayige alipata nafasi ya kuongoza mjadala wa kupata maoni, matarajio na matamanio ya Kampasi hii iweje au iwe na vitu gani muhimu kwa wana Kigoma.