




KATIBU MKUU UTUMISHI AFUNGUA MAFUNZO YA UONGOZI MUHAS
30 Mei, 2023
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Selemani Mkomi leo amefungua rasmi Mafunzo ya Stadi za Uongozi na Menejimenti kwa viongozi wa ndaki, Shule kuu, kurugenzi, vitengo na idara mbalimbali za Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, MUHAS.
Akizungumza katika ufunguzi huo, Katibu Mkuu, Bw. Juma Mkomi ameupongeza uongozi wa MUHAS kwa kuona umuhimu wa kutenga fedha na kugharamia mafunzo haya ambayo ni muhimu sana kwa viongozi waandamizi wa umma ili kuboresha utendaji serikalini.
Kwa kufanya hivi, Katibu Mkuu amesema uongozi wa MUHAS unakuwa umeitikia wito wa Serikali kwa kupitia Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakutenga fedha kuwapeleka watumishi kuhudhuria mafunzo.
“Nina imani kwamba mafunzo haya mnayoyapata yataenda kuongeza ufanisi katika maeneo yenu ya kutolea huduma mbalimbali”, Bw. Mkomi aliongeza.
Akitoa salamu za ukaribisho, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Andrea Pembe alieleza kuwa lengo la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo viongozi wa MUHAS kwenye nafasi zao mbalimbali ili kuboresha utendaji wao na kutoa huduma bora inayotarajiwa.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi kufungua mafunzo haya, Kaimu Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt Ernest Francis Mabonesho, alieleza kuwa pamoja na mada zingine washiriki wa mafunzo haya watajifunza masuala ya itifaki na ustaarabu, sheria ya utumishi wa umma, uendeshaji wa mashauri ya nidhamu, uongozi wa kimkakati, utaratibu wa kufanya maamuzi, utunzaji wa kumbukumbu za serikali katika utumishi wa umma na usalama wa taarifa za serikali.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanatolewa na wawezeshaji kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, TPSC na kufanyika kwenye ukumbi wa mikutano, MUHAS, jengo la CHPE.