








22 Mei 2023
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, akiwakilishwa na Prof. James Mdoe, Naibu Katibu Mkuu, leo amezindua rasmi Kamati ya Ushauri wa Viwanda (Industrial Advisory Board) ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) chini ya mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (Higher Education for Economic Transformation Project – HEET).
Akizungumza katika uzinduzi huu, Prof. Mdoe amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi kubwa za kukuza sekta ya elimu ya juu nchini kwa kuanzisha na kutekeleza mradi wa HEET. Akifafanua zaidi, Prof. Mdoe amesema kupitia utekelezaji wa mradi huu, serikali itaboresha mitaala, rasilimali-watu na mazingira ya kufundishia na kujifunza katika vyuo vikuu na taasisi mbalimbali za elimu ya juu 23.
“Kwa hapa MUHAS mradi utakarabati na kujenga Kampasi 2; Mloganzila na Kigoma, kuboresha miundombinu ya kujifunza na kufundishia, kuhuisha au kuandaa mitaala, kusomehs watumishi, kuweka miundombinu ya kisasa ya TEHAMA pamoja na kuweka mifumo ya kidijitali kwa ajili ya kufundishia na utawala pia” aliongeza.
Akiielezea Kamati hii kabla ya uzinduzi, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Andrea Pembe alisema kuwa kamati ina wajumbe wanaowakilisha waajiri, binafsi na umma, taasisi za utafiti, makampuni ya dawa, wahitimu wajasiriamali, wanataaluma wenye sifa maalum na wawakilishi wa wanafunzi.
Uzinduzi wa Kamati ya Ushauri ya Viwanda ya MUHAS ulienda sambamba na kufungua mafunzo ya mapitio ya mitaala kwa wanataaluma wa MUHAS.
Akifafanua zaidi Prof. Pembe amesema ilionekana kuwa inafaa Kamati hii ya Ushauri wa Viwanda izinduliwe wakati MUHAS inaendesha mafunzo ya mapitio ya Mtaala kwa wanataaluma. “Hii inaashiria dhamira halisi ambayo MUHAS inayo katika kuhakikisha kwamba mitizamo, maoni, na mahitaji ya soko yanazingatiwa wakati wa mapitio ya mitaala yetu”, aliongeza.
Uzinduzi huu pia uliudhuriwa na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Dkt. Harrison Mwakyembe, Kaimu Mkurugezi wa Elimu ya Juu, Dkt Kenneth Hosea, Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora, TCU, Dkt Telemu Kasile na waratibu wa kitengo cha kitaifa cha utekelezaji wa mradi wa HEET