Matukio katika picha wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge Elimu, Utamadunu na Michezo iliyoongozwa na Mwenyeki Prof. Kitulo Mkumbo ilipotembelea Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu kilichopo Kampasi ya Mloganzila.













Ijumaa Machi 17
Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imetembelea mradi wa Kituo Mahiri cha Afrika Mashariki cha Magojwa ya Moyo na Mishipa ya Damu kinachoendeshwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi, Muhimbili kilichopo kampasi ya Mloganzila na kujionea maendeleo ya kituo hicho ikiwa ni katika mikakati ya kukabiliana na magojwa yasiyoambukiza.
Akizungumza baada ya kumaliza ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Elimu, Utamaduni na Michezo. Prof. Kitila Mkumbo amepongeza kukamilika kwa awamu ya kwanza ya Kituo hiki Mahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu ikiwa ni pamoja vyumba vya kufundisha, maabara, kuandaa mitaala ya kufundishia wataalamu, manunuzi na uwekaji wa vifaa vya TEHAMA.
Akielezea umuhimu waliouona katika kukamilisha awamu ya pili ambayo ni ujenzi wa hospitali ya magonjwa ya moyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo amesema watalifikisha jambo hilo sehemu husika ili lifanyiwe kazi kwa haraka kuwezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo.
“Kwa sababu katika mafunzo ya udaktari darasa ni hospitali na tumeona kuna uhitaji huo na sisi kama kamati ya bunge elimu tutashauri serikali na tutawapitishia kamati ya afya ili waweke msisitizo katika hili’, alisema Prof.Mkumbo.
Vile vile mwenyekiti wa Kamati ya Bunge aliupongeza uongozi wa MUHAS kwa usimamizi mzuri wa mradi huu na kazi kubwa ya kuhakikisha elimu ya vyuo vikuu inakwenda vizuri.
“Kitu ambacho kimetufurahisha zaidi wanafunzi wanaosoma MUHAS wanapata ustadi wakujitegemea siyo tu kinadharia bali kivitendo kwa kujitegemea na hivyo kuweza kujiajiri na kutengeneza ajira kwa wengine”, aliongeza Mwenyekeiti wa Kamati.
Akileleza sababu ya uhitaji wa kuwa na hospitali ya magonjwa ya moyo, Mkurugenzi wa Kituo hiki, Prof. Gideon Kwesigabo alisema asilimia 37 ya vifo visivyotarajiwa nchini na Afrika ya Mashariki, hutokana na magonjwa ya moyo ambayo kama kungekuwa na matibabu ya uhakika na ya wakati, vifo hivyo vingezuilika. Alisema kuwa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla kuna uhaba mkubwa wa hospitali za moyo, Tanzania yenye watu millioni 60 ina kituo 1 kikubwa na 1 kidogo ambapo wastani unaoshauriwa ni sio chini ya kituo 1 kwa watu million moja.
Prof. Kwesigabo aliongezea kuwa ili Kituo hiki Mahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu kiweze kufanya kazi iliyokusudiwa, ni vema awamu ya pili ikapewa kipaumbele ili hatimaye Afrika ya Mashariki iweze kuwa na kituo kamili kama nchi zingine za Afrika ya Mashariki.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema serikali imefanya jambo kubwa katika kumaliza ujenzi wa awamu ya kwanza ambapo Kituo hiki kitaleta manufaa na mapinduzi katika sekta nzima ya elimu ya udaktari na kupunguza magonjwa na vifo vitokanavyo na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu na hivyo kuboresha ustawi na maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya watu wa Afika ya Mashariki.
Prof. Mkenda pia alisema kuwa Wizara yake tayari imeanza kulifanyia kazi suala la ujenzi na awamu ya pili wa Kituo hiki kwa sasa wako katika mazungunzo na Hazina kuweza kupata fedha kutoka Benki ya Afrika ili kuweza kukamilisha ujenzi huu.