




07 Machi 2023
Wafanyakazi wanawake wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, MUHAS na Kamati ya Chama cha Wafanyakazi THTU wametembelea wodi ya watoto waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kutoa msaada wa mahitaji muhimu kama sabuni, mafuta, taulo za watoto(pampers), dawa ya meno na maswaki ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanatakayofikia kilele chake tarehe 8 Machi.
Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Mratibu wa Kamati ya Wanawake THTU, Dkt. Restituta Mushi, amesema wanawake hao wameguswa kama wa mama na kuwakumbuka watoto kwa kufanya matendo ya huruma kwa kutoa msaada huu. “Tunaamini kabisa kwa msaada huu tuliotoa ni sehemu ndogo ya kuonyesha upendo kwa watoto wetu” amesema Dkt. Restuta
Aidha, Dkt. Restuta aliwashukuru wanawake wa MUHAS kwa kujitoa kwa michango yao iliyowezesha kununua mahitaji ya watoto hawa iliyokabidhiwa leo. Aliongezea kuwa baadhi ya michango iliwezesha kulipia gharama ya kipimo cha MRI kwa mtoto ambaye familia yake ilikuwa haina uwezo na kulipia gharama za mtoto mmoja ambaye kwa bahati mbaya alifariki na kumuwezesha mzazi kuweza kuchukua mwili kwa ajili ya mazishi
Kwa upande wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Meneja Afisa Muuguzi, Bi. Loveness Urassa ametoa shukrani na pongezi kwa wanawake wa MUHAS kwa msaada huo kwa kuwapa watoto kipaumbele. Amesisitiza kuwa uhitaji ni mkubwa na kuwataka waendelee kusaidia na wakijitokeza watu wengine bado wako tayari kuwapokea. “Mahitaji ni mengi kama kulipa gharama za matibabu kwa familia zisiyo na uwezo na hata ukarabati wa mazingira wanayoishi watoto hapa hospitalini”, alioongezea Bi. Loveness.
Naye Mratibu Mkuu wa Kamati ya Wanawake THTU Taifa, Bi. Salma Fundi alitoa shukrani zake kwa wanawake wa MUHAS kwa kuona umuhimu na upendo kwa kijitoa kwao ili kusaidia mahitaji ya watoto waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. “Niwaombe wamama wenzangu msiishie hapa muendelee na moyo huo huo watu wanamahitaji mengi sana”. Alisema Bi. Salma
Vile vile aliwashukuru wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa mapokezi mazuri wakati wa zoezi la ugawaji vitu na pia aliwatia moyo wazazi wanaouguza watoto wasichoke wazidi kupiga moyo konde.
Wanawake wa MUHAS walitembelea wodi ya watoto ya magojwa ya damu, utapiamlo, upasuaji na wodi ya saratani.