









MUHAS kupitia kitengo cha Programu ya Jinsia (Gender Program Unit) wamefanya semina ya mwongozo wa fani za afya na Sayansi Shirikishi kwa wanafunzi wa kike wanaosoma mchepuo wa sayansi (PCB na PCM) kwa shule za sekondari ili kufahamu kwa undani kuhusu fani za afya na kuwaongoza katika kufanya maamuzi ya fani wanazozitaka kusoma hapo baadae.
Mafunzo hayo yametolewa na Mhadhiri Kutoka MUHAS, Dkt. Hawa Mbawalla ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Programu ya Jinsia (Gender Program Unit) ambapo wanafunzi walipata elimu na muongozo wa kufikia ndoto za kuwa madaktari, wauguzi, wafamasia, madakatari wa meno, wataalamu wa maabara, wataalamu wa elimu ya jamii, jinsi ya kuchagua fani, jinsi ya kujiendeleza kitaaluma au fani na majukumu ya mwanafunzi wa masomo ya afya na sayansi shirikishi.
Vile Vile Mkuu wa Kitengo cha Udahili, Bi. Renista Mkoba aliwaelezea wanafunzi programu mbalimbali za afya na sayansi shirikishi zinazotolewa MUHAS na vigenzo vyake kuanzia ngazi ya Diploma mpaka Digrii na kuwasisitiza kusoma kwa bidii na malengo kulingana na fani wanazotaka kuchagua,
Naye Afisa mwandamizi wa TEHAMA, Bw. Andrew Katemi alitoa mada kuhusu umuhimu wa TEHAMA katika fani za afya na kuwasisitizwa wanafunzi kuwa wabunifu ili waweze kutatua changamoto zinazokabili jamii kupitia TEHAMA ambapo ndiyo dunia ya sasa ilipo na inapoelekea kwa kasi.
Mafunzo hayo yaliweza kuhudhuriwa na wanafunzi kutoka Baobao, St. Francis Girl’s, Cannosa, Loyola, Ifunda Tech, Jangawani, Al Muntazir, Hopac, Heritage, Pandahil, Marian Girls, Almis, Babro Johson, Ifakara, Msolwa Girls, Korogwe Girls, na Mazinde na pia wanafuzi walipata fursa ya kuuliza maswali na kuwashukuru watoa mada kwa kuwapa elimu ambayo imewasadia kufahamu kwa undani kuhusu fani za afya na sayansi shirikishi na itawaongoza katika kufanya maamuzi sahihi ya kuchagua fani wanazotaka.