










01 DESEMBA 2022
Watumishi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili waaswa kuchukua tahadhari na kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
Hayo yamesemwa leo tarehe 01 Disemba 2022 katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika Chuoni, MUHAS, yaliyohusisha watumishi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi, Muhimbili.
Akifungua maadhimisho hayo Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Appolinary Kamuhabwa ambaye alikuwa Mgeni Rasmi aliwasihi watumishi kutokufanya ngono zembe mfano kufanya ngono pasipo matumizi ya kinga na ameshauri watumishi kupima afya zao mara kwa mara.
“Chuo kimesaidia kuboresha mazingira ya makazi ya watumishi na wanafunzi ili kuhamasisha kuachana na ngono zembe kwa kusaidia kupatikana condoms, na kwa mwaka jana 2021 Chuo kimesamabaza jumla ya condoms mia tano nne (504) kwa watumishi na wanafunzi na tumeweza kufunga visambaza kondomu “condom dispenser” hamsini na sita (56) katika maliwato za watumishi na katika mabweni ya wanafunzi yaliyopo Muhimbili na Chole”, alisema Prof. Kamuhabwa.
“Ni wajibu wangu basi leo hii kuwakumbusheni, ni muhimu kupima na huduma hii inapatikana bure hapa Muhimbili. Kwa wale ambao wapo katika hali ya kupata watoto ni vizuri kupima wakati wa hali ya ujauzito ili hatua zichukuliwe na wataalamu ili kuzuia mtoto asije akazaliwa na maambukizi ya VVU ikiwa kama mama ameathirika”, aliongeza Prof. Kamuhabwa.
Maadhimisho haya pia yalihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Prof. Mohammed Janabi ambaye alipata nafasi ya kuwaelezea washiriki kuhusu UKIMWI ulivyokuwa miaka ya 90 na maendeleo yaliyopatikana mpaka sasa
Katika maadhimisho hayo watumishi wa MUHAS walipata fursa ya kusikiliza mada ya mabadiliko ya tabia iliyotolewa na Dkt. Garvin Kweka kutoka Hospitali ya Taifa, Muhimbili.
Madhumuni ya maadhimisho haya ni kutathmini hali na mwelekeo wa udhibiti UKIMWI Kitaifa na Kimataifa na siku hii hutumika kuhamasisha na kuelimisha Jamii juu ya namna ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU, matumizi sahihi ya ARV kwa watu wanaoishi na VVU pamoja na kupinga unyanyapaa na ubaguzi.
Kauli mbiu ya maadhimisho haya ya mwaka huu ni “IMARISHA USAWA” Ni kauli inayotutaka sote kwa pamoja tutekeleze afua za mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI kwa kuchukua hatua stahiki katika kutatua changamoto za ukosekanaji wa usawa katika mapambano ya kutokomeza VVU na UKIMWI