skip to Main Content
P.O. Box 65001, MUHAS,Dar es Salaam webmaster@muhas.ac.tz 0752360543 / 0756265177 - Admission Office

PICHA: Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Juma Kipanga alipotembelea banda la MUHAS kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa kwenye Maonyesho ya Biashara ya 46 ya Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba.

11 Julai, 2022

Naibu wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Juma Kipanga leo ametembelea banda la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi, Muhimbili (MUHAS) katika maonesho ya 46 ya biashara za kimataifa na kuelezea azma ya Serikali kupitia Wizara yake ya kuongeza udahili wa wanafunzi katika vyuo vikuu vya afya nchini.

Akizungumza baada ya kujionea kazi mbalimbali za udahili, tafiti na ubunifu zilizopo katika banda hilo, Naibu Waziri amesema kuna changamoto kwenye eneo la udahili wa wanafunzi katika sekta ya afya kwa sababu vyuo vilivyopo kwa sasa havina uwezo wa kuchukua idadi kubwa ya wanafunzi wenye sifa hasa kwenye sekta ya afya.

Akitoa mfano, Mhe Kipanga amesema kwa mwaka jana maombi ya wanafunzi waliotaka kuingia katika vyuo vikuu vya afya nchini yalikuwa ni zaidi ya wanafunzi 6000 hata hivyo uwezo wa vyuo vilivyopo hauzidi wanafunzi 2000. Hata hivyo Naibu Waziri alisema changamoto hii imeshachukuliwa na Serikali na kuangalia namna gani ya kuwawezesha wanafunzi hawa kupata fursa ya kuweza kusoma hapa hapa nchini.

Aidha Naibu Waziri amesema Serikali kupitia Wizara yake wamesaini mkataba na Benki ya Dunia  kwa ajili ya kuongeza ubora na udahili katika vyuo vyetu. “Kwa upande wa MUHAS peke yake tunaenda kujenga kampasi kubwa katika eneo letu la Mloganzila ambapo zaidi ya bilioni 80 zitatumika pale ili tuweze kuongeza udahili kwenye eneo hii” alisema Mhe. Kipanga.

Aidha Naibu Waziri aliongeza kuwa “Pia tunakwenda kujenga kampasi nyingine kule Kigoma kwa lengo hilo hilo la kuhakikisha kwamba tunaongeza udahili kwenye eneo hili hili la afya kwa sababu ni eneo ambalo tuna mahitaji nalo makubwa sana”

Pamoja na hayo Naibu Waziri aliwapongeza watafiti wa MUHAS kwa kufanya tafiti zinazohamasisha na kulenga matatizo yanakabili jamii ya Tanzania.

Ndani ya banda la Mhe. Kipanga alipata fursa ya kupewa elimu kuhusiana na ugonjwa wa siko seli na saratani ya damu na magonjwa ya kinywa kinywa na meno. Aliweza pia kujionea tafiti na mbambali ikiwemo tafiti za magonjwa na za tiba ya asili na kazi za ubunifu zinazofanywa na wanafunzi wa MUHAS

Maonesho haya maarufu yanayojulikana kama Maonesho ya Sabasaba yameanza kuanzia tarehe 28 Juni na yanatarajiwa kumalizika mnamo tarehe 13 Julai 2022.