



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Aldof Mkenda ametangaza motisha wa shilingi milioni 50 kwa watafiti wa sayasi na tiba watakaoweza kuchapisha matokeo ya tafiti zao kwenye majarida ya juu kabisa duniani.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Lupus Duniani yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof Mkenda amesema kuwa Serikali imeamua kuongeza nguvu kwenye elimu na tafiti za sayansi na tiba. “Sasa hivi Mhadhiri yoyote Mtanzania aliyepo kwenye chuo chochote cha umma au binafsi katika eneo la sayansi na tiba akiweza kuchapisha andiko lake la utafiti kwenye yale majarida ya juu kabisa kama Nature au Lancet, Serikali itampa shilingili million 50”, alisema Prof. Mkenda.
Akifafanua zaidi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema kuwa kama Serikali wameamua kufanya hivyo ili kuhakikisha kwamba wanajenga ushawishi kwa watafiti wa hapa nchini kuweka nguvu zao kwenye utafiti hali wakijua kwamba wanaweza kupata kipato na kuendeleza maisha yao kwenye utafiti.
Prof. Mkenda ameongeza kuwa hii itasaidia watafiti kutotapanya nguvu zao kufanya biashara na kazi mbalimbali kuongeza kipato ili kumudu maisha. “Tunataka tujenge mazingira kwa watafiti wetu hasa kwenye sayansi na tiba wafanye full time, kwa hiyo tumetenga bilioni moja kama motisha kwa kila atakayechapisha kwenye majarida hayo, haijalishi mko wangapi kila mmoja atabeba shilingi milioni 50”, aliongeza.
Aidha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema kuwa, Serikali pia imetenga fedha za kusomesha wahadhiri wa fani za tiba, sayansi na teknolojia kwenye vyuo bora nje ya nchi katika ngazi ya uzamili na uzamivu. Alisisitiza kuwa hela hizi za ufadhili zipo kwenye bajeti ya Wizara ambayo imepita kwa kishindo kikubwa hivyo wahadhiri wanaotaka kwenda kusoma wasisite kuziomba.
Akizungumzia Maadhimisho ya Siku ya Lupus Dunia, Prof. Mkenda alisema anahudhuria maadhimisho hayo kama mdau na kuungana na mashujaa wa lupus na familia zinazoishi na watu wenye ugonjwa wa Lupus kwa ajili ya kuendeleza ufahamu wa tatizo hili nchini. “Mimi ni mdau katika familia kwa hiyo nimeshaamua nitakuwa nakuja kuungana na nyie kila Mwenyezi Mungu atakavyoniwezesha kwa sababu kuja hapa ni kusaidia kusambaza taarifa hizi”, Prof Mkenda aliongeza.
Awali ya yote, akitoa salamu za ukaribisho Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Andrea Pembe alimshukuru Prof Aldof Mkenda kwa ketenga muda wake na kuja kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Lupus Duniani katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili na pia kutambua uwepo wake Chuoni hapo kwa mara ya kwanza tangia amekuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.