





Tarehe 04 Desemba, 2021
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameongoza sherehe za Mahafali ya 15 ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo kampasi ya Muhimbili.
Katika Mahafali hayo Rais Mstaafu aliwatunuku wahitimu 1,114 wa mahafali hayo stashahada, shahada za kwanza, shahada za uzamili na shahada za uzamivu katika fani mbalimbali za afya na sayansi shirikishi.
Akizungumza kabla ya kuwatunuku wahitimu hao, Mhe Dkt Kikwete aliwapongeza wahitimu wote kwa hatua waliyofikia na kuwahimiza kwenda kufanyakazi kwa bidii na maarifa ili kuisaidia Serikali ambayo imewekeza fedha nyingi kwenye sekta hiyo kwa kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za Afya.
“Nitoe rai kwenu ninyi wote mnaohitimu leo muende mkafanye kazi kwa bidii katika maeneo mbalimbali mtakayopangiwa na Serikali ili kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kwa kuboreshahuduma za Afya kwa kujenga miundombinu na kuimarisha huduma zaAfya”, alisema.
Aidha Mhe. Dkt Kikwete amebainisha kuwa kuna idadi ndogo ya wahitimu wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika vyuo vikuu vya hapa nchini tofauti na nchi nyingine za Afrika Mashariki, hivyo ameutaka uongozi wa MUHAS kuweka mipango maalum ya kuwasaidia wanafunzi wenye sifa na uwezo wapate fursa ya kuendelea na masomo ili kupata wataalamu wa kutosha kwenye vyuo na taasisi za elimu ya juu hapa nchini.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Dkt. Harrison Mwakyembe, amesema kuwa miongoni mwa mambo yaliyopo katika mpango mkakati wa Chuo hicho nikuongeza udahili wa wanafunzi, kuongeza ubora wa mafunzo na ufundishaji, kuwaongezea uwezo watafiti ili kuwa na ubora zaidi, kuboresha miundombinu ya kufundishia, kuboresha Maktaba pamoja na miundombinu ya TEHAMA.
“Tunapenda kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi (Higher Education and Economic Transformation – HEET) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia wenye lengo la kukisaidia Chuo katika ujenzi wa madarasa, kampasi ya Mloganzila,” Dkt Mwakyembe aliongeza.
Akiwaelezea wahitimu wa mwaka huu kabla hawajatunukiwa shahada na stashahada mbalimbali, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Andrea Pembe alisema kuwa wahitimu 201 watatunukiwa stashahada na stashahada ya juu, wahitimu 535 shahada ya kwanza, wahitimu 354 shahada ya uzamili, wahitimu 20 shahada za uzamili za utaalamu (Super specialty) na wahitimu 4 watatunukiwa shahada za uzamivu.