skip to Main Content
P.O. Box 65001, MUHAS,Dar es Salaam webmaster@muhas.ac.tz 0752360543 / 0756265177 - Admission Office
Makamu Mkuu wa Chuo Prof.Andrea Pembe akifungua kongamano la miaka 60 ya Uhuru lililo fanyika Chuoni, MUHAS
Baadhi ya Washiriki wa Kongamano la Miaka 60 ya Uhuru Wakisikiliza Hotuba ya Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Andrea Pembe (hayupo kwenye picha).
Jopo la Wataalamu Kutoka Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili MUHAS Wakijadili na Kufanya Tathmini ya Mwenendo wa Magonjwa na Mwitikio wa Sekta ya Afya Nchini Katika Kongamano la Miaka 60 ya Uhuru Lililofanyika Chuoni.
Mmoja wa Washiriki Prof. Bruno Sunguya Akichangia Mada Iliyojadiliwa Katika Kongamano la Miaka 60 ya Uhuru Lililofanyika Chuoni MUHAS.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili MUHAS Akizindua Kitabu Kinachoelezea Historia ya Uuguzi Ambacho Kimeandikwa na Prof. Edith Tarimo Katika Kongamano la Miaka 60 ya Uhuru Lililofanyika Chuoni
Viongozi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shilikishi Muhimbili MUHAS Wakiwa Katika Picha ya Pamoja na Washiriki wa Kongamano la Miaka 60 ya Uhuru Lililofanyika Chuoni.

Katika kuadhimisha sherehe za miaka 60 ya Tanzania Bara, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili kwa kushirikana na Chuo Kikuu cha Dodoma na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Ndaki ya Mbeya wamefanya Kongamano MUHAS ambapo mada kuu ilikuwa ni Miaka 60 ya Uhuru: Mabadiliko ya Magonjwa na mwitikio wa Sekta ya Afya nchini.  

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano hilo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Prof. Andrea Pembe ameeleza kuwa ongezeko la watu limepelekea mabadiliko katika kada ya afya ambapo kabla na baada ya uhuru kulikua na magonjwa ya kuambukiza ila kwa sasa kumekuwa na magonjwa mengi ya mlipuko na yasiyoambukiza.

“Wakati wa uhuru watu walikua milion 9 na sasa hivi ni takribani milion 60 na asilimia kubwa ya watanzania wanaishi mjini hali hiyo imepelekea mabadiliko mbalimbali ikiwemo chakula, Wingi wa watu na aina ya maisha yamesababisha kutokea kwa magonjwa ya mlipuko na yasiyo ambukiza kama shinikizo la damu, kisukari, n.k”, Prof. Pembe alisema

Prof Pembe aliongeza kuwa Makongamano kama haya ni muhimu katika sekta mbalimbali ili tuweze kujadili na kutafakari kwa pamoja wapi tumetoka, wapi tumefika na wapi tunaelekea kama Taifa la Tanzania tokea tulipopata Uhuru miaka 60 iliyopita. “Tafakuri kama hii inatusaidia sisi kama wadau katika sekta mbalimbali nchini kuweza kuona wapi tumefanya vizuri, wapi tulipokosea na wapi tunahitaji kuweka msisitizo zaidi ili kufikia malengo tuliojiwekea kama Taifa,” Prof. Pembe alieleza.

Akiongelea maendeleo ya MUHAS tangu kilipoanzishwa miaka 2 baada ya uhuru kama Shule ya Tiba ya Dar es Salaam, Prof. Pembe amesema kuwa Chuo kimeendelea kukua na kupanua mazingira ya ufundishaji na utafiti huku kikichukua nafasi kubwa katika kutoa ushauri wa kitaaluma kwenye masuala ya afya kwa taasisi mbalimbali, serikali yetu na kwa jumuiya ya kimataifa.

Makamu Mkuu wa Chuo huyo alieleza kuwa mwaka huu, Chuo  kinategemea kuadhimisha hatua nyingine muhimu ya kukamilika kwa Awamu ya kwanza ya ujenzi wa Kituo cha Afrika Mashariki cha Umahiri cha Moyo na Mishipa ya Damu (East African Centre of Excellency in Cardiovascular Sciences) katika kampasi ya Mloganzila. Alisema Kituo hicho kitafunguliwa rasmi siku ya Jumatatu tarehe 6 Desemba na Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa Chuo, Kituo hiki kitatoa mafunzo na kuzalisha rasilimali watu katika taaluma bobezi (specialists na super specialist) za moyo na mishipa ya damu kwa nchi za Afrika Mashariki.  “Hii inaonyesha kwa kiasi gani kama nchi tumeweza kupiga hatua katika kipindi hiki cha miaka 60 ya Uhuru hasa katika mafunzo ya wataalam wa afya hapa nchini,” aliongeza.

Katika Kongamano hilo washiriki waliweza kujadili mada mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya kiepidemiolojia kutoka kabla ya uhuru hadi baada ya uhuru ambayo iliyoongozwa na Prof. Japhet Killewo; mabadiliko ya kidemografia na kiuchumi na athari zake kwa afya ya watanzania ambayo iliwasilishwa na Dkt. George Ruhago; na  wajibu wa vyuo vikuu katika kushughulikia changamoto za kiafya za ndani ya nchi na ulimwenguni ambayo ilioongozwa na Prof. Eligious Lyamuya.