








Tarehe 06 Desemba 2021.
Makamu wa Kwanza wa Rais Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe Othman Masoud Othman amefungua Kituo cha Afrika Mashariki cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu (The East African Centre of Excellence for Cardiovascular Sciences) cha Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shrikishi Muhimbili katika kampasi ya Mloganzila.
Akizungumza katika sherehe za ufunguzi wa Kituo hicho kilichojengwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Mhe Othman alisema amefurahishwa na maendeleo yaliyopatikana tangu mazungumzo ya awali ya uanzishwaji wa Kituo hiki yalipofanyika mwaka 2012. Aliongeza kuwa anaamini uwekezaji uliofanyika ni wa faida kubwa kwa Serikali na kwa wananchi pia hasa ukizingatia takribani kila kaya hapa nchini imeathirika na magonjwa haya ya moyo na Kituo hiki kimekusudia kushughulikia matatizo hayo.
“Kituo hiki kitatoa mafunzo mbalimbali ya rasilimali watu wa afya ambayo wanahitajika kwa ajili ya kuzuia na kuhudumia magonjwa ya moyo na mishipa damu na kwa kufanya hivyo, tutaweza kukabiliana na changamoto ya upungufu wa rasilimali watu wanaohitajika katika maeneo haya”, Mhe Othman aliongeza.
Ufunguzi wa Kituo cha Afrika Mashariki cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali ikiwa ni pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akiwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, viongozi wa taasisi mbalimbali za serikali na mwakilishi kutoka benki ya Maendeleo ya Afrika.
Kwa mujibu wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe Prof. Joyce Ndalichalo Kituo hiki kimejengwa kimkakati katika kampasi hii ya Mloganzila na kinalenga kukuza ujuzi na elimu ya juu katika sayansi za biomedikali (Skills Development and Tertiary Education in Biomedical Sciences) ili kuweza kuchangia katika maendeleo ya watumishi wanaohitajika na wenye ujuzi wa hali ya juu katika sayansi za biomedikali na hivyo kukidhi mahitaji ya haraka ya soko la ajira la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Katika kufanikisha mradi huu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliingia mkataba wa mkopo kwa masharti nafuu na Benki ya Maendeleo ya Afrika ambapo Benki ilitoa TZS 18,623,125,000.00 ikiwa ni sawa na asilimia 92.58 na Serikali ya Tanzania iliridhia kutoa TZS 1,489,850,000.00 ikiwa ni sawa na asilimia 7.42 kama ufadhili wa serikali” Prof. Ndalichako alieleza.
Sambamba na hayo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikihi, Muhimbili, Prof. Pembe alieleza kuwa kituo hiki kina vyumba vya madarasa, semina, ukumbi wa mikutano, kumbi za makongamano kwa njia ya video, chumba cha mafunzo kwa njia ya mtandao, maktaba, chumba cha takwimu, (data management centre), maabara nne kwa ajili ya tafiti, na za mafunzo kwa vitendo pamoja na ofisi za wanafunzi wauzamivu na za wafanyakazi.
“Katika kuandaa walimu watakaofundisha katika kituo hiki, mradi umetoa mafunzo kwa wataalam wapatao 38 na kati ya hao wataalam wapatao 29 wamemaliza na wanaendelea kutoa mafunzo na huduma katika taasisi mbalimbali za afya hapa nchini” Prof. Pembe alieleza.
Aliongeza kuwa pamoja na kwamba kituo hii kitakuwa chini ya Chuo, kitafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili kutekeleza sera, taratibu na miongozo ya huduma za afya na wakati huo huo kikitekeleza sera, taratibu na miongozo ya Elimu ya juu kama zilivyoainishwa na Wizara zote mbili.
Aidha katika Ufunguzi wa Kituo hiki, Mhe Othman aliwasihi watanzania kujitahidi kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kugundua magonjwa mapema ili yaweze kutibiwa mara moja. Pia alisisitiza kuzingatia njia mbalimbali za kinga hasa kwa magonjwa ya moyo na mishipa damu ambayo ni ghali sana kutibu na yana kawaida ya kuwa na matokeo mabaya ikiwa hayatatibiwa kwa wakati.
“Napenda kuchukua fursa hii kuwahakikishia wanajumuia wa MUHAS kwamba serikali itaendelea kuwaunga mkono katika kuhakikisha hospitali ya moyo ya kufundishia wataalam kwa vitendo inajengwa ili Kituo hiki kiweze kukamilika kama ilivyokuwa imepangwa,”, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar aliongeza.