MAKAMU MKUU WA CHUO AFUNGUA UCHAGUZI WA WAJUMBE WA KUCHAGULIWA WATAKAOUNDA BARAZA LA WAFANYAKAZI LA MUHAS
28 Aprili 2021
Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Andrea Pembe leo amefungua uchaguzi wa wajumbe wa kuchaguliwa watakaounda Baraza la Wafanyakazi wa MUHAS.
Akizungumza na wafanyakazi wa MUHAS kabla ya uchaguzi huo, Prof Pember alisisitiza umuhimu wa zoezi hilo. “Kwa ujumla uchaguzi huu ni muhimu sana kwa wafanyakazi ili wapate wawakilishi sahihi katika Baraza la Wafanyakazi ambao watawasilisha mawazo yao kuhusu namna bora ya kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya wafanyakazi ili kuwezesha Chuo kufikia malengo yake.”, Prof. Pembe alisema.
Uchaguzi huo ulitanguliwa na wafanyakazi kupewa elimu kuhusu umuhimu wa Baraza la Wafanyakazi mahali pa kazi na kutambua umuhimu wa kuchagua wawakilishi sahihi watakaounda Baraza la Wafanyakazi la MUHAS. Elimu hii ilitolewa na Mtaalam kutoka Ofisi ya Kamishna wa Kazi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu.
Akizungumzia matarajio ya mkutano huo Prof. Pembe amesema ni kutoa elimu fupi kwa wafanyakazi kuhusu umuhimu wa Baraza la Wafanyakazi katika kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya watumishi ili kufikia malengo ya kazi.
Na vile vile ni kuweza kutambua na kuchagua wawakilishi sahihi ambao watawasilisha changamoto zinazowakabili wafanyakazi katika utendaji pamoja na mapendekezo ya namna ya kutatua changamoto hizo ili ziweze kufanyiwa kazi na Uongozi wa Chuo.
Uchaguzi huo umefanyika chini ya usimamizi wa Mtaalam kutoka Ofisi ya Kamishna wa Kazi iliyo katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Kurugenzi ya Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala pamoja na waangalizi kutoka Vyama vya Wafanyakazi vya RAAWU na THTU.